[Latest Updates]: Tanzanite kuwa na hati ya utambulisho Kimataifa

Tarehe : Aug. 31, 2018, 7:29 a.m.
left

Na Asteria Muhozya, Dodoma

Serikali imesema inafanya utaratibu wa kuwa na Hati ya Utambulisho wa Kimataifa wa Madini ya Tanzanite, ambayo yanapatikana katika nchi ya Tanzania pekee katika vilima vya Mirerani, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ushauri na Uchambuzi wa Kazi kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Nolasco Kipanda, akiwasilisha mada kuhusu Muundo na Majukumu ya Wizara ya Madini na Tume ya Madini.[/caption]

Hayo yamebainishwa leo tarehe 25 Agosti na Waziri wa Madini Angellah Kairuki wakati wa Semina ya mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo imefanyika Makao Makuu ya Wizara, jijini Dodoma.

Waziri Kairuki amesema kuwa, serikali inataka kuona kuwa dunia inafahamu kuwa, madini hayo yanapatikana Tanzania pekee na kuhakikisha kwamba yanajulikana zaidi.

Semina ya wabunge imefanyika kufuatia maelekezo ya Kamati hiyo ambayo ilitaka kufahamu kuhusu mwenendo mzima wa Madini ya tanzanite, biashara na udhibiti wa madini hayo baada ya kujengwa kwa Ukuta wa Mirerani unaozunguka migodi ya madini ya tanzanite, Muundo wa Wizara ya Madini, Tume ya Madini na majukumu yao.

Waziri Kairuki amesema kuwa, Wizara imepata fursa ya kuwasilisha kwa Kamati hiyo taarifa za utekelezaji wa majukumu mbalimbali ikiwemo mikakati ya serikali katika kudhibiti utoroshaji wa madini hayo na mipango madhubuti ambayo serikali inakusudia kuifanya ili kuhakikisha kwamba rasilimali madini inalinufaisha taifa na hatimaye sekta ya madini iweze kufikia asilimia 10 ya machango wake katika pato la taifa ifikapo mwaka 2025.

Ameongeza ni  kikao ambacho kimekuwa na manufaa kwa upande wa Serikali kwa kuwa imetoa elimu kwa Kamati hiyo kuhusu yale ambayo serikali imefanya na inayokusudia kufanya kuhusuiana na madini  ya tanzanite lakini pia serikali imepata wasaa wa kupokea maoni, mapendekezo na maelekezo kutoka kwa wabunge ambayo yatawezesha kupeleka mbele sekta ya Madini.

Mbali ya tanzanite, Waziri Kairuki amewaeleza wabunge hao kuhusu mkakati wa serikali kuanzisha Mineral Exchange ambapo amesema tayari wizara imeshaandaa timu ya wataalam ili kwenda kujifunza na kufanya utafiti katika nchi nyingine ili suala hilo liweze kufanyika kwa ubora.

Sehemu ya Maafisa Waandamizi wa Wizara na Tume ya Madini wakifuatilia mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.[/caption]

Pia, ameeleza kuwa, Wabunge wa Kamati hiyo, wamepata fursa ya kufahamu majukumu ya Wizara baada ya kuundwa kwa Tume ya Madini, majukumu ya tume ya madini na mahusiano ya kiutendaji kati ya Tume na Wizara.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mariam Ditopile, amesema kuwa, kamati imebaini kuwa, Serikali imechukua hatua nyingi za kulinda na kudhibiti madini ya tanzanite ikiwemo  kudhibiti utoroshaji wa madini hayo. “Kama kamati tumeona mnyororo mzima wa thamani ya madini ya tanzanite, awali tulikuwa hatunufaiki kama taifa,” amesema Ditopile.

Awali, akiwasilisha mada kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kudhibiti utoroshaji wa madini ya tanzanite na usimamizi wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini ndani ya ukuta, Afisa Madini Mkazi wa Mirerani Mhandisi David Ntalimwa, amezungumzia sababu za kushuka kwa mapato na kueleza kuwa, kunategemea kiwango cha ubora na sifa za madini husika.

Ameongeza kuwa, kutokana na mazingira hayo, kiwango cha thamani ya madini na tozo ya mrabaha kitakuwa tofauti kutegemea na mwezi na uzalishaji uliopo.

Akizungumzia sababu za utoroshaji wa madini ya tanzanite, Mhandisi Ntalimwa amesema kuwa, zinatokana na uwezo mdogo wa kusanifu na kuongeza thamani na kunga’risha madini ya vito na hivyo watu kutamani kuuza tanzanite ghafi.

Pia, amesema utoroshaji wa madini unatokana na kukwepa kulipa kodi na tozo mbalimbali zinazotozwa na serikali ili kujipatia faida kubwa, kuwepo kwa raia wa kigeni nchini wanaofanya biashara ya madini kinyume na sheria kwa kushirikiana na wazawa na kukosekana kwa masoko ya uhakika ya kuuzia madini yanayozalishwa.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na serikali katika kudhibiti utoroshaji wa madini baada ya kujengwa ukuta amesema kuwa, serikali imeimarisha ulinzi na ukaguzi getini kwa kutumia vikosi vya ulinzi na usalama, kuzuia magari kuingia na kutoka ndani ya ukuta, watu kuingia ndani ya ukuta kwa vitambulisho maalum.

“ Sasa watu wanaingia kwa utaratibu maalum tofauti na walivyozoea awali. Ukuta umeleta utaratibu mzuri na si kero, kama baadhi ya watu wanavyodhani,” amesisitiza Ntalimwa.

Amezitaja hatua nyingine kuwa ni pamoja na kuzuia Mabroker kwenda migodini na badala yake kutakiwa kusubiria madini getini, uthaminishaji madini kufanyika ndani ya ukuta na serikali kujenga jengo lenye ofisi ya ukaguzi, uthaminishaji na ukumbi wa mabroker ndani ya ukuta.

Aidha, pamoja na kushiriki semina hiyo, pia wabunge hao wamepata fursa ya kutembelea Makumbusho ya Taifa ya Jiolojia na Madini katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania, (GST).

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals