Tarehe : June 23, 2026, 2:34 p.m.
Prof. Shemdoe: Hatua hiyo itaongeza ufanisi wa utendaji na kusaidia kutatua changamoto za wananchi na watumishi
Azindua rasmi Mfumo wa NGAO na Daftari la Huduma za Serikali (GSD)
Wizara ya Madini na Taasisi zake zajidhatiti kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na wadau wa Sekta ya Madini
Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, amezitaka Wizara, Idara, Wakala na Taasisi za Umma nchini kuunganisha huduma wanazozitoa kupitia mifumo ya Serikali ya kidijitali ili kurahisisha utoaji wa huduma na kuimarisha uwajibikaji kwa wananchi.
Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo leo Juni 23, 2026, wakati akifunga rasmi Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma kuanzia Juni 16, 2025.
Amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali yameendelea kuleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za umma kwa kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa haraka, kwa urahisi na kwa uwazi zaidi, huku yakipunguza urasimu na gharama za upatikanaji wa huduma.
Aidha, amesema maadhimisho ya mwaka huu yamefanikiwa kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa kuwapatia huduma na taarifa mbalimbali moja kwa moja, jambo lililosaidia kutatua changamoto zao na kupunguza malalamiko yaliyokuwa yakijitokeza kuhusu utoaji wa huduma katika taasisi za umma.
Katika hatua nyingine, Prof. Shemdoe amezindua rasmi Mfumo wa NGAO pamoja na Daftari la Huduma za Serikali (Government Service Directory – GSD), mifumo inayolenga kuboresha uratibu wa huduma za Serikali, kuongeza uwazi na kurahisisha wananchi kupata taarifa na huduma mbalimbali za umma.
Sambamba na hilo, amewataka Wakuu wa Taasisi na Maafisa Rasilimali Watu kutenga muda wa kusikiliza changamoto za watumishi na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati ili kuongeza morali ya kazi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, amesema jumla ya taasisi 226 zimeshiriki Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu, hatua inayoonesha kuongezeka kwa mwitikio wa taasisi za umma katika kuwafikishia wananchi huduma na taarifa muhimu.
Amesema Serikali imeendelea kutumia maonesho hayo kama jukwaa la kuonesha mafanikio yaliyopatikana katika utoaji wa huduma kwa wananchi, miradi ya maendeleo inayotekelezwa pamoja na uwekezaji uliofanywa katika kuboresha utendaji wa utumishi wa umma.
Aidha, amebainisha kuwa zaidi ya taasisi 500 tayari zimeunganishwa na kutumia mifumo ya Serikali ya kidijitali katika utoaji wa huduma, jambo ambalo limechangia kuimarika kwa huduma za umma, kuongeza uwazi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Wizara ya Madini pamoja na taasisi zake zimeshiriki katika maadhimisho hayo kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa katika sekta ya madini, fursa za uwekezaji, shughuli za utafiti wa madini, usimamizi wa rasilimali madini pamoja na mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa Taifa.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2026 yameongozwa na kaulimbiu isemayo:
“Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu.”
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.