[Latest Updates]: Zambia Yavutiwa na Maendeleo ya Sekta ya Madini Tanzania

Tarehe : Nov. 20, 2025, 1:51 p.m.
left

Dodoma

Ujumbe kutoka Zambia unaoongozwa na Balozi wa Zambia nchini Tanzania, Balozi Matthews Jerre, umepongeza na kuvutiwa na maendeleo ya sekta ya madini nchini Tanzania, hususan namna shughuli za uchimbaji na mtandao wa vituo vya ununuzi na masoko vinavyoendeshwa kuanzia ngazi ya Wachimbaji Wadogo hadi Wakubwa, pamoja na uwepo wa sera thabiti inayotoa miongozo na usimamizi wa rasilimali za madini.

Hayo yalisemwa Novemba 20, 2025 na Balozi wa Zambia nchini Tanzania, Matthews Jerre, mapema baada ya kupokea wasilisho maalum kuhusu mwenendo wa uchimbaji, usimamizi, masoko, sheria na taratibu za uwekezaji chini ya Sera ya Madini ya Mwaka 2009.

Akizungumzia kuhusu mifumo ya usimamizi wa masoko, Tisa Chama ambaye ni Afisa Fundi Mkuu kutoka Kampuni ya Umma ya Zambia ya ZCCM-IH inayowakilisha Serikali katika kampuni za madini na nishati, aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuweka mifumo thabiti inayounganisha masoko yote na vituo vya ununuzi wa madini — jambo ambalo Zambia inatamani kufikia ili kujua kiwango halisi cha dhahabu kinachozalishwa.

Kwa upande wake, Kennedy Mwandama, Afisa Biashara Mkuu wa ZCCM-IH, alivutiwa na matumizi ya teknolojia katika mifumo ya masoko ya madini, ushirikishwaji wa wachimbaji wadogo katika shughuli za utafiti na uchenjuaji kwa kufuata ushauri wa kitaalamu pamoja na miongozo mbalimbali ya kisekta inayounganisha sekta binafsi na Serikali.

“Binafsi nimevutiwa sana na matumizi ya teknolojia katika mifumo ya masoko na vituo vya ununuzi wa madini katika maeneo mbalimbali ya nchi. Hii ni faida kubwa kwa wadau na taifa kwa ujumla, na ni hatua kubwa sana ya maendeleo,” alisema Mwandama.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Madini, Archard Kalugendo, aliuelezea ujumbe huo kuwa Tanzania iliamua kurasimisha wachimbaji wadogo ili kutambua mchango wao mkubwa. Hadi sasa, wachimbaji wadogo wanachangia takribani asilimia 40 ya mapato ya sekta ya madini, na mwaka 2024 sekta ya madini ilichangia asilimia 10.1 katika Pato la Taifa.

Kalugendo alifafanua kuwa mageuzi makubwa yalianza baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2017, ambapo kanuni mbalimbali zilizotungwa zilipelekea kuanzishwa kwa masoko rasmi ya madini na vituo vya ununuzi nchi nzima.

Pamoja na mambo mengine, Kalugendo aliupongeza ujumbe huo kwa kutambua changamoto zao, hasa katika uchimbaji na usimamizi wa dhahabu, na kuamua kuja Tanzania kujifunza.

Mbali na wasilisho hilo, ujumbe huo ulitembelea kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Eyes of Africa kilichopo Dodoma ili kujionea utendaji kazi, ikiwemo matumizi ya teknolojia katika usafishaji wa dhahabu.

Naye, mmiliki wa kiwanda hicho cha Eyes of Africa, Ference Molnar, aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wamiliki wa viwanda vya kusafisha dhahabu, hususan katika kushirikiana na wachimbaji wadogo pamoja na taasisi za fedha ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals