[Latest Updates]: Tume ya Madini yatangaza zabuni ununuzi wa maeneo yenye leseni hodhi za madini

Tarehe : Dec. 19, 2019, 8:42 a.m.
left

Na Greyson Mwase, Dodoma

Tume ya Madini  imetangaza zabuni kwa ajili ya ununuzi wa maeneo  10 yenye leseni hodhi za madini  na yenye ukubwa wa kilomita za mraba 381.89 yaliyopo katika maeneo ya Ngara – Kagera, Kahama- Shinyanga, Chunya- Mbeya, Bariadi na Busega – Simiyu, Morogoro, Nachingwea – Lindi ambayo awali leseni hodhi zake zilikuwa zimerudishwa Serikalini.

Uamuzi huo umetangazwa leo tarehe 19 Desemba, 2019 na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula kupitia mkutano wake na waandishi wa habari  uliofanyika  jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Kamishna wa Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya pamoja na watendaji wengine wa Tume ya Madini.

Profesa Kilula alifafanua kuwa, awali mwaka 2017 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Madini Sura Namba 123 na kanuni zake ambapo  pamoja na mambo mengine, zilizokuwa leseni  hodhi za madini ( retention licence) zilirudishwa  Serikalini .

Alisema baada ya marekebisho hayo maeneo yote 10  yenye ukubwa wa kilomita za mraba 381.89 yalirudishwa Serikalini na kuongeza kuwa, wachimbaji wa madini wengi wamekuwa wakiulizia maeneo hayo mara kwa mara lengo likiwa ni kuomba leseni za uchimbaji madini.

Aliendelea kusema kuwa, baada ya uchambuzi wa kina kufanyika, Serikali kupitia  Tume ya Madini, maeneo yote 10 yaliyokuwa na leseni hodhi yatatolewa kwa zabuni na kukaribisha kampuni za uchimbaji wa madini na watu binafsi  wenye uwezo wa fedha na utaalam katika miradi ya uchimbaji wa madini  na wenye nia ya kuendeleza miradi ya madini ya nickel, dhahabu na rare earth elements kuomba zabuni hizo.

Aliongeza kuwa, mwekezaji atakayeonesha nia ya kuwekeza katika maeneo hayo atakuwa na jukumu  la kufanya kazi na kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini.

Wakati huo huo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya akielezea hatua zinazochukuliwa kwa wamiliki wa leseni  wasioendeleza maeneo yao, aliwataka wamiliki  na waombaji wote wa leseni  za utafutaji na uchimbaji wa madini  wenye mapungufu kurekebisha mapungufu  hayo ndani ya  siku 30 kuanzia sasa.

Alifafanua mapungufu hayo kuwa ni pamoja na leseni ambazo hazifanyiwi kazi, leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango la mwaka, maombi ambayo hayajalipiwa ada ya maombi na maombi yaliyokosa viambatisho muhimu kwa mujibu wa sheria.

Profesa Manya alitaja mapungufu mengine kuwa ni pamoja na waombaji waliokidhi vigezo vya kupewa leseni lakini hawajalipa ada ya maandalizi na wamiliki ambao leseni zao zimeshatolewa lakini hazijachukuliwa.

Alifafanua kuwa mpaka sasa leseni zaidi ya 134 za utafutaji na uchimbaji wa kati wa madini hazijachukuliwa na zaidi ya maombi 450 ya leseni za utafutaji yana mapungufu.

Akielezea hatua zitakazochukuliwa kwa kampuni au watu binafsi walioaminiwa na Serikali na kupewa leseni lakini wameshindwa kutekeleza masharti ya leseni kwa mujibu wa Sheria ya Madini,  alisema leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango kwa mwaka, leseni ambazo hazifanyiwi kazi na leseni ambazo zimekwishatolewa lakini hazijachukuliwa zitaandikiwa hati ya makosa na yasiporekebishwa zitafutwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha alisema kuwa, maombi yote ya leseni za utafutaji na uchimbaji wa kati yenye mapungufu yataondolewa kwenye mfumo wa utoaji wa leseni ili waombaji wengine wenye sifa pamoja na wachimbaji wadogo waweze kuomba maeneo hayo.

Aliendelea kusema kuwa, maombi ambayo yamekidhi vigezo vya kupewa leseni lakini hayajalipiwa ada ya kuandalia leseni yataondolewa kwenye mfumo ili waombaji wengine wenye sifa waweze kuomba maeneo hayo.

Alisisitiza kuwa tangazo la zabuni husika linapatikana katika tovuti ya Wizara ya Madini ambayo ni (www.madini.go.tz)  Tume ya Madini (www.tumemadini.go.tz) magazeti ya Habari Leo na Daily News ya tarehe 20 Desemba, 2019 pamoja na blogs na mitandao ya kijamii.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals