[Latest Updates]: Dkt. Mpango Azindua Nishati Mbadala Mkaa wa kupikia

Tarehe : Aug. 12, 2022, 2:36 p.m.
left

Dkt. Mpango Azindua Nishati Mbadala Mkaa wa kupikia

Ø  Atoa Maagizo kwa Wizara ya Madini, Kazi, STAMICO, Tume ya Madini, NEMC

Ø  Apongeza Mageuzi yaliyofanywa STAMICO, yapunguza utegemezi

Ø  STAMICO yatoa Gawio la Tsh. Bilioni 2.2 kwa Serikali

Ø  Rais Samia Atuma Salam za Pongezi

Asteria Muhozya, Bibiana Ndumbaro na Steven Nyamiti- Dodoma

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amezindua  nishati mbadala ya kupikia inayotokana na makaa ya mawe na kueleza kuwa italeta mapinduzi  makubwa na kusaidia kupunguza athari za uharibifu wa mazingira zinazotokana  na matumizi ya mkaa unaotokana na miti.

Aidha, Dkt. Mpango amelipongeza Shirika hilo kwa kupunguza utegemezi kutoka Serikalini kutoka asilimia100 hadi asilimia kufikia asilimia 13  na kuyataka mashirika mengine kujifunza kutoka kwa STAMICO kutokana na historia ambayo shirika hilo limepitia ikiwemo kuwa miongoni  mwa mashirika yaliyotaka kufutwa na Serikali .

Ameyasema hayo wakati akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya STAMICO ya kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1972 huku taifa likishuhudia mageuzi makubwa ya kiuchumi na kiuwekezaji yaliyofanywa na shirika hilo kwa kipindi cha miaka michache.

Kufuatia mafanikio hayo, amelitaka shirika hilo kutobweteka badala yake kuendelea kufanya kazi kwa juhudi kwa niaba na manufaa ya watanzania ili waweze kunufaika ipasavyo na rasilimali madini ambazo nchi ya Tanzania imejaliwa kuwa nazo na kuongeza kwamba, ni asilimia10 tu ya madini ambayo yameguswa na kutumia fursa hiyo kuwahamasisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania kuwekeza katika sekta ya madini.

Pamoja na kutoa pongezi hizo, Makamu wa Rais amesema ipo changamoto ya kuongezeka kwa magonjwa ya vumbi  yanayotokana na shughuli za madini ambapo takwimu zinaonesha vijana wenye umri kati ya miaka 20- 40 wameathirika na vumbi hilo huku serikali ikitumia gharama ya shilingi milioni 500 kwa mwaka  kwa ajili ya matumizi ya mitungi ya hewa kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo hayo.

Kufuatia athari hizo, Makamu wa Rais ametoa agizo kwa Wizara ya Madini, Mikoa, viongozi wa Vyama vya wachimbaji kuwatembelea wagonjwa wanaokabiliwa na changamoto ya maradhi hayo katika hospitali ya Kibongo’to ili kujionea hali halisi na kuchukua hatua madhubuti.

Aidha, ameigiza Wizara ya Madini Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu na Wizara ya Afya kushirikiana ili kuwa na Sheria itakayowezesha afya na usalama katika shughuli za uchimbaji madini zinazingatiwa hivyo kubidhiti changamoto za magonjwa yanayotokana na shughuli hizo.

Pia, amezitaka kampuni zote zinazochimba madini kuendelea kutunza mazingira ya migodi na kutengeneza upya maeneo ya uchimbaji baada ya shughuli za uchimbaji kukamilika badala ya kuacha mashimo na kuiagiza Tume ya Madini,  Wizara na  Baraza la Taifa  la  Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC ) na  kuongeza bidii katika kufanya kaguzi migodini na kusisitiza kuendelea kutolewa kwa elimu kuhusu afya na usalama  migodini na umuhimu wa matumizi ya barakoa

Pia, ameiagiza Tume ya Madini kusaidia upatikanaji wa fedha na vitendea kazi kwa ajili ya kuboresha mazingira ya shughuli za wachimbaji wadogo. Huku akiitaka STAMICO kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kubuni na kutengeneza zana bora na zenye teknlojia rahisi kwa wachimbaji ili kuwawezesha kuzalisha kwa tija.

Halikadhalika, ameitaka Wizara na STAMICO kuhakikisha zinakomesha ajira kwa watoto katika shughuli za migodi ili kuwawezesha kuendelea na masomo na hivyo  kushiriki katika kujenga taifa imara.

Awali, akitoa salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu, amesema Rais Samia amelipongeza shirika hilo kwa kutimiza miaka 50 ya kuanzishwa kwake na kueleza kuwa, Serikali yake itaendelea kuiimarisha STAMICO na kwamba inalitupia jicho suala la wafanyakazi na masuala yanayohusu taratibu za ununuzi.

Naye, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko akizungumza katika hafla hiyo amesema kuwa, miradi mingi ya shirika hilo tayari imefufuliwa ukiwemo wa Kiwira ambao  ulisimama tangu mwaka 2008 na kueleza kuwa, kutokana na juhudi zilizofanywa na shirika hilo tayari limekarabati miundombinu kwa mgodi wa chini ambapo zaidi ya kilomita 4.4 zimekamilika. Pia, amesema shirika limekarabati nyumba zipatazo 100 kati ya 300 na kuongeza kuwa, shirika limefanikiwa kutoa ajira zipatazo 700 kwa watanzania.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo amelitaka shirika hilo kuhakikisha watanzania wanatumia mkaa wa Rafiki Briquettes kutokana na umuhimu wake ili kusaidia kutunza mazingira uhifadhi wa mazingira.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini  Seif Gulamali   amesema  Shirika hilo limepiga hatua na limefanya Mapinduzi makubwa ndani Muda mfupi  ukilinganisha na lilivyokuwa kabla ya mwaka 2018.

 Aidha, ameipongeza Bodi na Menejimeti ya STAMICO  kwa kuwa wasikivu na waelewa  katika kufuata maagizo ya Kamati.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse Akizungumza kuhusu historia ya STAMICO, amesema ilianzishwa ili kuhakikisha Serilkali inashiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa uchimbaji madini ukianzia kwenye utafiti hadi hatua ya kupata madini. 

 Amesema shirika hilo lina historia na limepitia mabadiliko mengi tangu kuanzishwa kwake 1972 hadi ilipofika na kuhuhishwa tena mwaka 2015 ambapo lilifanyiwa maboresho ya kimuundo na kiuongozi

 Amesema STAMICO ina muundo wa tofauti ukilinganisha na miundo ya mashirika ya madini katika baadhi ya nchi za Afrika zinazojihusisha na shughuli za madini, akitolea mfano nchi ya Zambia na Angola, ambapo STAMICO imeongezewa jukumu la kuwalea wachimbaji wadogo ambalo inaendelea kulitekeleza kwa bidii.

 Amesema STAMICO inatekeleza jukumu hili kwa kutoa elimu ya vitendo,  kutoa vifaa vya kutendea kazi ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wanashiriki katika uchumi jumuishi wa madini na kuleta maendeleo kwao binafsi na Taifa. 

 Naye, Katibu Mkuu wa Chama Cha Wachimbaji Wanawake Tanzania (TAWOMA) Salma Ernest amesema, STAMICO ni taasisi ambayo imeonesha kwa vitendo kuwa ni mlezi bora kwa wachimbaji na imekuwa ni msaada na kimbilio kwa wachimbaji wadogo katika kutatua changamoto kwa haraka sana.

 Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini   Tanzania (FEMATA) John Bina ameipongeza STAMICO kwa kutimiza miaka hamsini (50) na kuongeza kuwa shirikisho hilo lina imani na STAMICO kuendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wachimbaji wananufaika na rasilimali madini za nchi.

 Ameiomba STAMICO kuchukua hatua ya kuwaendeleza mafundi mchundo kwa kuwapa teknolojia mpya za uchimbaji zinazoingia hapa nchini ili waweze kuiga na kuzitumia teknolijia hizo kwa manufaa ya shughuli za uchimbaji na hivyo kuongeza tija.

 

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals