[Latest Updates]: Kituo cha Madini na Jiosayansi Kunduchi, kinavyowanufaisha Watanzania

Tarehe : March 26, 2019, 2:52 p.m.
left

TAARIFA za kijiolojia zinaonesha kuwa, Afrika ni bara lenye utajiri mkubwa wa rasilimali madini huku sehemu kubwa ya madini hayo yakiwa bado hayajaanza au yako kwenye hatua mbalimbali za uendelezaji.

Aidha, rasilimali za madini zilizopo barani Afrika hususani Tanzania, taarifa za kijiolojia zinadokeza kuwa yanaweza kuwa ni chanzo kikubwa cha kuharakisha maendeleo ya kiuchumi kwa Taifa na kijamii ikiwa kila mmoja aliyepewa jukumu la kuwajibika katika sekta ya madini atatumia utaalamu wake, weledi na ufanisi ili kupata matokeo chanya.

Ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Magufuli kwa kutambua utajiri mkubwa wa madini tuliyonayo hapa nchini yakiwemo ya tanzanite, almasi,dhahabu, chuma au vito ameendelea kutoa hamasa kwa viongozi wenye mamlaka ya kuyasimamia madini kuongeza ubunifu na usimamizi wenye tija.

Kwa kutambua umuhimu wa madini katika kuharakisha maendeleo ya nchi, Wizara ya Madini kupitia viongozi wake kila kukicha wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali ili kutumia fursa zilizopo ndani na nje ya nchi kuleta tija kubwa kwenye sekta ya uchimbaji wa madini, uongezaji wa thamani na usimamizi wa sekta kwa matokeo makubwa.

           WAZIRI NYONGO

Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, ameshiriki katika kikao cha 39 cha kutathmini utendaji wa Kituo cha Madini na Jiosayansi cha Afrika (AMGC)) katika kutekeleza maazimio ya nchi wanachama kilichofanyika nchini Sudani Februari 18, mwaka huu.

Neno jiosayansi linamaanisha sayansi inayohusu Dunia ikihusisha masuala yote yanayohusisha elimu ya miamba kama vile utafutaji wa madini, uchimbaji, uchenjuaji pamoja na biashara ya madini.

Hivyo, AMGC ni kituo kinachoratibu masuala hayo kwa nchi mwanachama wa umoja huo katika Bara la Afrika.

Kituo hicho kilichoanzishwa na Kamisheni inayohusu masuala ya Kiuchumi katika Umoja wa Afrika (UNECA) kwa lengo la kusimamia na kuratibu shughuli zote zinazohusu sekta ya madini chini ya Mwamvuli wa Dira ya Afrika kuhusu Madini (AMV) ili kupelekea maendeleo endelevu kwa nchi wanachama pasipo kuathiri mazingira. 

Umoja huo ulianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1977 ukijulikana kama Southern and Eastern African Mineral Centre (SEAMIC) ambapo shughuli zake zilikuwa zikifanyika katika jengo la Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) jijini Dodoma, kabla ya kuhamia katika ofisi zilizopo Kunduchi jijini Dar es Salaam. 

Gharama za ujenzi wa ofisi za kituo hicho zilitokana na michango ya nchi wanachama.

Aidha, kituo hicho kinafanya shughuli mbalimbali za madini ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya namna ya kukata na kuchenjua madini, kukata madini na kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na madini, uchambuzi na huduma za ushauri katika maeneo tofautitofauti ya kimadini, pamoja na tafiti juu ya madhara yatokanayo na kemikali za kuchenjulia madini kwa mazingira. 

Kabla ya mkutano uliowahusisha mawaziri wenye dhamana na sekta ya madini, kulitanguliwa na mikutano mingine miwili iliyohusisha Bodi ya Wakurugenzi wa kituo hiki ni kikao kidogo zaidi wakiwa ni wasimamizi wa karibu wa kituo kikao cha pili kinawahusisha watendaji wakuu katika wizara zenye dhamana ya madini, ambacho baada ya kikao waliwasilisha taarifa za kikao katika mkutano wa Baraza la Mawaziri la nchi wanachama kwa ajili ya kutolea maamuzi.

Kuhudhuria katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Madini Nyongo amesema, amejifunza namna sekta ya madini nchini Sudan ulivyojipanga katika kuikwamua Sudan kiuchumi kutokana na rasilimani madini. 

Ameendelea kueleza kuwa, nchi ya Sudan inazalisha madini ya dhahabu kwa wingi kwa kiasi cha tani 107 ukilinganisha na Tanzania inayofikisha kiasi cha takriban tani 50 kwa mwaka.

Nyongo anaeleza kuwa, kiasi cha tani 107 cha dhahabu kilichozalishwa nchini Sudan mwaka uliopita kiliuzwa nje ya nchi ambapo asilimia 90 ya madini hayo yalichimbwa na kuuzwa kutoka kwa wachimbaji wadogo. 

Waziri Nyongo amekiri kuwa, sekta ya uchimbaji mdogo inao uwezo mkubwa wa kuchangia katika pato la Taifa tofauti na fikra za wengi zilivyo.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia uwajibikaji wa migodi katika kutoa huduma na unufaikaji wa wazawa, Torence Ngole amesema uwepo wa kituo hicho kwa Watanzania una manufaa makubwa kwa Watanzania hususani wachimbaji wadogo katika kujipatia ujuzi.

Lakini pia kituo hicho kina maabara kubwa inayotumika katika kuchunguza madini na kuyabainisha ambapo wachimbaji wanaweza kupeleka madini yao na kuwa na uhakika zaidi wa mali waliyonayo. 

Katika kupunguza migogoro katika kanda ya maziwa makuu kama vile Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi zenye migogoro na vita, Ngole amebainisha uwepo wa mashine maalumu inayoyafanya uchunguzi wa madini na kubaini madini hayo yanachimbwa nchi gani. 

Amesema, ikibainika kuwa madini husika yanapatikana katika nchi zenye vita basi hayapewi kibali cha kuweza kuyauza na hivyo kuyanyima sifa ya kuuzika. 

Hiyo ni moja kati ya mbinu ya kuleta amani na kupunguza kasi ya mauaji miongoni mwa nchi katika Bara la Afrika.

Pamoja na kuiwakilisha nchi katika kikao hicho cha mwaka, Ngole amesema alipata fursa ya kutembelea maonesho ya madini yanayoandaliwa na wizara yenye dhamana na madini nchini Sudan na kujifunza mambo muhimu ambayo nchi yetu ikiyafanya itasaidia katika kukuza sekta ya madini.

Amesema, kuwepo kwa maonesho ya madini kunafungua ukurasa kwa wachimbaji na wauzaji wa madini kukutana na kushirikishana uzoefu katika masuala yanayohusiana na sekta ya madini. 

Swali unaweza kujiuliza je? Umoja wa kusimamia sekta ya madini Afrika una umuhimu gani?. 

Akifafanua swali hilo, Ngole anasema, wakati wa uumbaji wa nchi/dunia mipaka ya kikanda na kijiografia havikuwepo, kutokana na hilo mipaka hiyo haizuii miamba ya madini iliyopo Tanzania inapofika baina ya mpaka wa nchi na nchi kukoma na kutokuendelea, kutokana na ukweli huo ushirikiano huo utazifanya nchi mwanachama kufanya shughuli za uchimbaji kwa namna zinazofanana na kutumia uzoefu wa nchi jirani kutambua uwepo wa madini katika nchi nyingine. 

Ameongeza kuwa, katika kufanya tafiti za madini kuna ramani za madini zinatengenezwa, endapo kutakuwa na ushirikiano ramani hizo zitaandaliwa kwa vigezo vinavyofanana hivyo utangazaji wa sekta ya madini kufanana kwa nchi zote mwanachama.

Ameendelea kueleza kuwa, tafiti za pamoja zinasaidia sana katika kugundua aina mbalimbali za madini yaliyopo kwenye nchi wanachama kutokana na kufanya tafiti kwa pamoja na kubainisha kuwa mipaka ya kijiolojia iko tofauti na mipaka ya kijografia.

Pia ushirikiano unasaidia kupunguza changamoto ya utoroshwaji wa madini na kubainisha kuwa kutokuwepo na ushirikiano na mbinu za kuwafanya watoroshaji wa madini kukaguliwa katika mipaka ya nchi, nchi mwanachama hazitanufaika na madini yanayochimbwa kwani hayatalipiwa tozo zinazotakiwa na Serikali.

Katika hatua nyingine, inabainishwa kuwa, ushirikino ukiwepo baina ya nchi wanachama nchi hizo zitakuwa na sera zinazofanana kusimamia sekta ya madini. 

Hii itatokana na mijadala wanayoifanya ya kubaini na kuchangia uzoefu katika kuendesha sekta, wawekezaji watashindwa kukimbia kimbilia, kwani sera zinafanana za nchi hizo zinafanana na kuamua kuwekeza mahali walipoanzia.

 UMOJA UNAVYOJIENDESHA

Uendeshwaji wa kituo hicho unategemea michango ya nchi wanachama kwa asilimnia 60 ambapo kila nchi mwanachama anatakiwa kuchangia kiasi cha sh.milioni 150 (zaidi ya dola za Kimarekani 62,000) kwa mwaka na asilimia 40 zinatokana na kipato kitokanacho na ada za huduma zinazotolewa na kituo hicho.

        KILICHOJADILIWA

Aidha, katika kikao hicho, kilijadili tathmini ya utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na kikao cha maamuzi cha mwaka uliotangulia ili kujiridhisha na mwenendo wa kituo hicho na kubaini changamoto zinazopelekea maagizo hayo kutokutekelezwa.

UMUHIMU WA KITUO

Kwanza kabisa kituo cha umoja huo kipo nchini Tanzania katika Jiji la Dar es Salaam. Uwepo wa kituo hicho ni heshima kubwa taifa limepewa na kuaminiwa na nchi wanachama.

Umuhimu wa kwanza unaotokana na kituo ni elimu inayotolewa katika kituo hicho kwa wachimbaji wadogo wa madini, hivyo Watanzania wengi kunufaika. 

Wachimbaji wanafundishwa namna ya kukata madini, kuyaongezea thamani kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na madini pamoja na njia bora za uchenjuaji wa madini.

Pili kituo kinatoa huduma za kimaabara, hivyo mtu yeyote mwenye madini na anataka kutambua madini yake anaweza kupata huduma hiyo katika kituo hicho.

 

Vikao vya utendaji wa kituo vinakaliwa kila mwaka sawasawa na utaratibu uliowekwa na nchi wanachama.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals