[Latest Updates]: Naibu Waziri Nyongo Afunga Mitambo Yote ya Kuchenjulia Madini Kahama

Tarehe : March 31, 2019, 3:55 p.m.
left

Na Greyson Mwase, Kahama

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amefunga mitambo yote ya kuchenjulia madini ya dhahabu Wilayani Kahama baada ya kubaini udanganyifu mkubwa kwenye uchenjuaji wa madini.

Naibu Waziri Nyongo amechukua hatua hiyo kwenye ziara yake aliyoifanya mapema leo tarehe 31 Machi, 2019 Wilayani Kahama yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha, Kamishna Msaidizi, Uendelezaji Migodi na Madini wa Wizara ya Madini,  Ali Saidi Ali, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Andrea Fabian, wataalam kutoka Tume ya Madini, wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na waandishi wa habari.

Akiwa katika ziara hiyo, alifanya ziara ya kushtukiza katika kampuni ya kuchenjua madini ya dhahabu ya Ng’ana Group inayomilikiwa na  Theogenes Zacharia pamoja na mwenzake aliyejulikana kwa jina la  Antidius na kubaini kampuni hiyo imekuwa ikiwaibia wateja wake kupitia mfumo wa uchenjuaji wa madini ya dhahabu.

Akiwa ameambatana na msafara wake mara baada ya kuwasili katika kampuni hiyo alioneshwa na wataalam kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini waliopewa kazi maalum ya kuchunguza mfumo wa uchenjuaji wa dhahabu wa kampuni hiyo, sehemu ya mabomba ya mfumo iliyoharibiwa kwa makusudi kwa lengo la kunasa kiasi cha dhahabu kabla ya kufikishwa katika chombo maalum cha kupokelea kwa ajili ya mteja.

Alisema kuwa, kiasi cha kaboni iliyokuwa na dhahabu iliyokamatwa ilipelekwa kwa ajili ya kuchenjuliwa ili kubaini kiasi cha adhabu kilichokuwa kimeibiwa na kusisitiza kuwa baada ya kuchenjuliwa kiasi cha gramu 102 kiligundulika kutaka kuibwa.

Katika hatua nyingine mbali na kufunga mitambo ya kuchenjua madini ya dhahabu katika Wilaya ya Kahama, Naibu Waziri Nyongo alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya ya Kahama kuhakikisha watuhumiwa wote wa kampuni ya Ng’ana Group wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Aidha, Naibu Waziri Nyongo alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila kumsimamisha kazi mara moja Kaimu Afisa Madini wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama na uchunguzi kuanza mara moja.

Katika hatua nyingine, Nyongo alisema kuwa maafisa madini wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama wataanza kufungua mtambo mmoja mmoja wa kuchenjua madini ya dhahabu mara baada ya kujiridhisha na uendeshaji wake.

Awali akielezea siri ya wizi unaofanywa na kampuni ya  Ng’ana Group, mmoja wa wateja kutoka kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya  Joseph Magunila & Partners, aliyepeleka kaboni kwa ajili ya kuchenjuliwa ili kupata madini ya dhahabu, Wema Shibitali alisema kuwa, wakati zoezi la uchanjuaji likiendelea alishangaa kupata kiasi kidogo cha dhahabu tofauti na kaboni iliyokuwa imewekwa.

Alisimulia kuwa aliomba maafisa kutoka vyombo vya dola kufungua mfumo ili kubaini kama kuna madini yamebaki na kuongeza kuwa mara baada ya mfumo kufunguliwa walibaini kiasi kikubwa cha kaboni kilichokuwa kimebaki kwenye mfumo.

Aidha Shabitali aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuwatetea wachimbaji wadogo kwa kuwa wamekuwa wakiibiwa na wachenjuaji wa madini ya dhahabu kwa muda mrefu.

Wakati huo huo akizungumza katika msafara huo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha mbali na kumpogeza Naibu Waziri Nyongo kwa kutembelea Wilaya yake na kushughulikia changamoto mbalimbali kwenye Sekta ya Madini, alisema kuwa ziara hiyo imewapa mwanga zaidi wa mbinu zinazotumiwa na wachenjuaji wa madini na kusisitiza kuwa ataendelea kusimamia kwa karibu zaidi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Aliwataka wachimbaji na wachenjuaji wa madini nchini kuunga juhudi zinazofanywa na Rais wa Awamu ya Tano pamoja na Serikali yake, Dkt. John Pombe Magufuli katika kulinda rasilimali za madini kwa kuwa waaminifu kwenye ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali za Serikali.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals