[Latest News]: Waziri Aweso Ataka Tafiti za Wanajiosayansi Kutoka Matokeo Chanya

Tarehe : Oct. 7, 2022, 10:36 a.m.
left

WAZIRI AWESO ATAKA TAFITI ZA WANAJIOSAYANSI KUTOA MATOKEO CHANYA*

 

 

*Wanajiosanyansi waiomba Serikali mfumo wa kuwasilisha ushauri wao kwenye uendeshaji Sekta za Madini, Nishati, Maji, Ujenzi na nyinginezo*

 

*Atambua  mchango wa Wataalam wa Maji nchini, asema wana nguvu ya kulisaidia Taifa*

Kamishna wa Madini Dkt. Mwanga asisitiza mfumo kudhibiti taarifa za jiolojia

Asteria Muhozya na Kisonga Jackson - Arusha

Waziri wa Maji Jumaa Aweso ametaka wanaojiosayansi nchini kufanya tafiti ambazo zitatoa matokeo chanya na kuhimiza zifanyike kwa weledi, ujuzi na maarifa ili ziwezeshe kuchochea uchumi wa nchi na maendeleo ya watu.

Kauli ya Waziri Aweso imezingatia umuhimu wa taaluma hiyo na mahitaji ya jamii ambayo hutoshelezwa kwa kutumia rasilimali za asili zinazopatikana nchini na duniani ambapo sehemu kubwa wanajiosayansi ndiyo wataalam wanaoshiriki katika kutafuta na kuvuna rasilimali hizo.

Ameyasema hayo Oktoba 6, 2022 wakati akifunga Mkutano wa Jumuiya ya Wajiolojia Tanzania (TGS) uliofanyika jijini Arusha na kushirikisha wanajiosayansi kutoka sekta mbalimbali zikiwemo za Madini, Nishati, Maji, Vyuo Vikuu, kampuni binafsi na taasisi za umma.

Ametolea mfano wa rasilimali asilia ambazo zimepatikana kutokana na mchango wa wanataaluma hao ambazo zimeliwezesha taifa kunufaika ipasavyo kiuchumi, kimaendeleo na kijamii na kutaja baadhi kuwa ni uwepo wa gesi asilia inayozalishwa mkoani Mtwara ambayo imesaidia kuzalishwa kwa nishati ya umeme, uwepo wa miradi mbalimbali ya madini inayotekelezwa nchini yakiwemo madini adimu ya Tanzanite yanayopatikana Tanzania pekee duniani na miradi ya maji ambayo imewezesha  huduma hiyo muhimu kwa watu.

Kufuatia umuhimu wao kwa taifa, amewataka kuungana na kuwa na chombo rasmi kitakachosaidia kuondokana na wababaishaji ili hatimaye utaalamu wao uwe kimbilio la Serikali.

Akizungumzia mchango wa wataalam wa maji katika maendeleo ya nchi, amesema wamesaidia kuondoa tatizo la maji kwa kumtua mama ndoo kichwani kwa kusaidia upatikanaji wa mita za ujazo  bilioni 126  kati yake  mita za ujazo bilioni 105 zikiwa  juu ya ardhi na mita za ujazo  mita  bilioni 21 chini ya ardhi.

Pia, ametaja maeneo kadhaa nchini ambayo awali hayakuwa na huduma hiyo lakini kutokana na mchango wa wataalam hao nchini wamefanikisha upatikanaji wa maji katika maeneo ya Buhingwe  mkoani Kigoma ambapo maji kiasi cha lita elfu 40 kwa saa zimepatikana, pia yamepatikana katika maeneo ya Liwale mkoa wa Lindi na maeneo mengine nchini ikiwemo miradi mbalimbali ya maji ambayo imewezesha wananchi kupata  huduma za maji

“Wahaidrojia wana nguvu ya kusaidia taifa na mnaweza kuhakikisha malengo ya Serikali yanafanikiwa, ninawapongeza sana,’’ amesisitiza Waziri Aweso.

Kufuatia hatua hiyo, amewataka kuungana na kuwekeza katika teknolojia za kisasa ili kusaidia kuondoa changamoto za upatikanaji wa maji na visima vya kutosha nchini.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Elisante Mshiu amesisitiza kwa kuiomba Serikali kuwezesha uwepo wa mfumo wa kuhakiki utoaji ajira kwa watalaamu kutoka nje ya nchi ili kuhakikisha  Kanuni za Local Content zinazingatiwa na kueleza ‘’suala hilo litafanyika kwa kushirikiano baina ya Bodi ya Wajiolojia, Idara ya kazi na Uhamiaji’’.

Vilevile, amependekeza kuwepo mfumo  rasmi wa wanajiosayansi kuwasilisha mawazo na ushauri serikalini hususan kwenye uendeshaji wa Sekta za  Nishati,  Madini, Maji, Ujenzi wa Miundombinu, Utunzaji wa Mazingira, Usalama Migodini, Kilimo, Afya, Elimu na Viwanda.

‘’Chama kinapendekeza kuanzishwa mfumo wa kuishauri Serikali kitaalam kuhusiana na uendeshaji wa sekta zilizoanishwa  ikiwa ni pamoja na kutoa maoni ya namna bora ya kuwa na Sheria na Kanuni rafiki zitakazohamasisha ukuaji wa sekta mbalimbali pamoja na namna bora  ya kuendesha uvunaji wa malighafi zilizoko nchini ili kukuza viwanda nchini,’’ amesisitiza Dkt. Mshiu.

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Prof. Abdulkarim Mruma ametoa ombi  kwa Serikali kupitia Waziri wa Maji kulifanyia kazi suala la kuwepo kwa mfumo utakaowaruhusu wataalam hao kutoa mawazo kwa Serikali kwa mustakabli wa maendeleo ya Sekta  muhimu za kiuchumi kwa maendeleo ya Taifa na vizazi vijavyo na kuongeza kwamba, wao kama wanajiosayansi wako tayari kuisadia  Serikali.

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amesisitiza suala la kuwepo kwa mfumo wa kudhibiti utoaji wa taarifa za kijiolojia ili zisaidie katika maendeleo ya nchi hususan katika masuala ya uwekezaji nchini.

‘’ Tunatakiwa kuwa na macho ya kuona madini, mfumo wa kudhibiti taaluma ni muhimu kwani taarifa hizi zitasaidia katika maendeleo ya nchi,’’ amesema Dkt. Mwanga.

Mkutano huo ambao umefungwa leo, katika kipindi chote uliendeshwa chini ya kaulimbiu *Mkakati wa Kutengeneza Mazingira Bora ya Uwekezaji katika Sekta za Madini, Maji na Nishati*

 

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals