Tarehe : June 8, 2023, 9:22 a.m.
Zikiwa zimetimia Siku 100 tangu ateuliwe na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Februari 27, 2023 kuiongoza Wizara ya Madini, Juni 7, 2023, Katibu Mkuu Kheri Mahimbali akizungumza na Watumishi wa Wizara, aliwaeleza Mikakati Kabambe inayolenga kuifanya Sekta ya Madini Kuzalisha Zaidi.
Mahimbali alibainisha mikakati mbalimbali inayolenga kuifungamanisha Sekta ya madini na sekta nyingine kubwa kiuchumi ili ikuze uchumi, ichangie zaidi fedha za kigeni na iongeze mchango wake katika Pato la Taifa.
Mahimbali aliyataja maeneo ambayo tayari wizara imeanza kuweka msukumo na kuimarisha uhusiano katika utekelezaji wake ni pamoja Kilimo, Nishati, Mawasiliano na kueleza kwamba, kama taifa linayo madini ambayo yanaweza kutumika kuzalisha mbolea suala ambalo litapunguza gharama ya kuagiza mbolea kutoka nje na kusema kuwa, zaidi ya shilingi bilioni 700 zinatumika kununua mbolea kutoka nje.
Alitaja eneo lingine kuwa ni kuhakikisha huduma ya nishati inafika katika maeneo ya migodi ili kuongeza uzalishaji wa madini na kuwawezesha wachimbaji kuchimba kwa tija.
Akieleza uhusiano wa wizara na sekta nyingine katika kuboresha mazingira ya shughuli za uchimbaji alisema, kutokana na ushirikiano ambao umefanywa na wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati, umewezesha Mgodi wa dhahabu wa STAMIGOLD wa Biharamulo ulio chini ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kufikiwa na huduma ya nishati ya umeme na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji.
Pia, amesema baada ya STAMIGOLD, Mgodi wa kuzalisha dhahabu wa Geita ambao umekua ukitumia gharama kubwa za uzalishaji kutokana na kukosa huduma hiyo muhimu uko mbioni kuunganishwa na nishati ya umeme.
Vilevile, alilitaja eneo lingine la kimkakati kuwa ni mawasiliano ambapo alisema lengo la wizara ni kuhakikisha migodi yote nchini inafikiwa huduma ya mawasiliano ya mtandao suala ambalo litaongeza tija kwenye shughuli za madini.
‘’ Tutakwenda wizara moja baada ya nyingine ili kuhakikisha kwamba Sekta ya madini inakwenda kufungua milango ya kiuchumi kwenye sekta hizi. Kwenye elimu tunataka kuhakikisha wanafunzi wanaosoma masomo yanayohusu sekta hii wanapata nafasi za mafunzo kwenye migodi ili kuwajenga waifahamu mapema sekta ya madini kwa vitendo,’’ amesisitiza Mahimbali.
Akizungumzia mikakati ya kuendeleza madini muhimu na mkakati ambayo yanayohitajika sana kwa sasa duniani kutokana na umuhimu wake, amesema, tayari wizara imeanza na itahakikisha inaweka nguvu kubwa katika uendelezaji wa madini hayo ikiwemo kuendeleza rasilimaliwatu.
Aidha, amesema wizara itashirikiana na wadau mbalimbali katika kufanikisha shughuli za utafiti wa madini hayo.
Vilevile, amewahakikishia watumishi wa wizara kuendelea kuboresha maslahi yao na kuweka mazingira bora ya kazi.
Akifungua kikao hicho, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko alimpongeza Katibu Mkuu Mahimbali kwa kuandaa kikao hicho ambacho pia kimelenga kupima utendaji wa wizara kwa siku tajwa.
Aliwataka watumishi wa Wizara kwa kipindi hiki kuelekea Mwaka Mpya wa Mwaka wa Fedha 2023/24 kuhakikisha wanajipanga kutekeleza malengo ya bajeti ili kuwezesha yale yaliyopangwa kutekelezwa yanatokea.
Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu ana matarajio makubwa na Sekta ya madini ya kuiona sekta hiyo inakua kichocheo kikuu cha uchumi wa Taifa.
Aidha, alisema katika kipindi hiki ambacho mataifa kadhaa yamekumbwa na changamoto ya ukosefu wa fedha za kigeni, ni wakati muafaka kwa Sekta ya Madini nchini kuhakikisha inalinusulu taifa lisikumbwe na changamoto hiyo na kuongeza kwamba, hivi sasa sekta ya madini inachangia zaidi ya asilimia 56 ya fedha za kigeni zinazotokana na mauzo ya bidhaa nje ya nchi.
Kutokana na matarajio hayo, amewataka watumishi wa Wizara ya Madini kujipanga na kuhakikisha kila mtumishi anayaelewa malengo na vipaumbele vya wizara na kutekeleza wajibu huo kwa moyo wa uzalendo huku wakiacha alama.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.