[Latest Updates]: Kiwanda cha Mayanga, Mkombozi Wachimbaji Wadogo wa Dolomite Kwedikwazu

Tarehe : Sept. 15, 2025, 3:05 p.m.
left

 Handeni, Tanga

Imeelezwa kuwa Kiwanda cha Mayanga kinachojihusisha na uchakataji wa madini ya dolomite kilicho Handeni mjini, mkoani Tanga, kimekuwa mkombozi mkubwa kwa Wachimbaji Wadogo wa kijiji cha Kwedikwazu na maeneo jirani, baada ya kuwapatia soko la madini hayo.

Awali, wachimbaji hao walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya kuuza madini yao kwa bei ya kusuasua pamoja na kulazimika kuyasafirisha mbali na kupelekea faida kidogo, hali iliyopelekea wachimbaji wa mawe hayo meupe kutoona manufaa makubwa ya kazi zao. 

Wakizungumza na Madini Diary hivi Karibuni, Wachimbaji na wafanyabiashara wa madini hayo walieleza kuwa, kupatikana kwa kiwanda hicho pamoja na vingine kumesaidia kuimarisha mnyororo wa thamani wa madini ya dolomite, huku wachimbaji wakipata kipato chenye tija zaidi sambamba na uhakika wa masoko.

“Kupatikana kwa Kiwanda cha Mayanga kumetupa matumaini makubwa kama wachimbaji wadogo. Sasa tuna uhakika wa soko na bei nzuri ukilinganisha na zamani tulipokuwa tunahangaika kusafirisha madini hadi mbali. Tunaishukuru serikali na wadau kwa hatua hii.” Alisema Ashura Mohamed, mchimbaji mdogo wa dolomite Kwedikwazu.

Aidha, wakazi hao walitoa wito kwa Serikali na wadau wa maendeleo kuendelea na ujenzi wa viwanda ili kutoa ajira pamoja na uhakika wa masoko ya mazao ya madini kama mawe hayo yanayotumika kwa ajili ya ujenzi, malighafi ya mbolea, rangi za majengo, malighafi za viwandani pamoja na urembo.

“Kiwanda hiki kimefungua milango si tu kwa wachimbaji, bali hata sisi wafanyabiashara wadogo wa madini, tunaiomba Serikali na wadau wengine waendelee kuwekeza katika ujenzi wa viwanda zaidi, ili kuongeza masoko na kuongeza thamani ya rasilimali zetu.” Alisisitiza Rajabu Makamba, mfanyabiashara wa madini ya dolomite Handeni.

Mbali na faida hiyo, kiwanda cha Mayanga kimefungua fursa nyingi za ajira kwa wakazi wa Handeni, hususan vijana, ambao sasa wanajihusisha na shughuli za uchimbaji, usafirishaji, uchakataji na kazi nyingine zinazohusiana na uendeshaji wa kiwanda. Hatua hiyo imechangia kupunguza tatizo la ajira na kuinua hali ya maisha ya familia nyingi zinazozunguka mradi huo.

Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda hicho Leonard Kimaro maarufu Mayangwa alibainisha kuwa uwepo wa kiwanda hicho pia umechochea ukuaji wa biashara ndogondogo na huduma mbalimbali katika maeneo ya jirani, ikiwemo usafirishaji, malazi na chakula, hivyo kuongeza kasi ya mzunguko wa fedha katika wilaya ya Handeni.

“Sisi tunazalisha chokaa, malighafi ya kutengeneza rangi na mbolea, kwa sasa soko letu kubwa lipo ndani ya nchi, lakini tunafikiria kuongeza uzalishaji na hatimaye kuanza kufikiria kujitanua zaidi katika masoko ya nje ya nchi kwa siku zijazo” alisema Kimaro.

Naye, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga, Mhandisi Laurent Bujashi alieleza kuwa Serikali imeendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa uwekezaji hapa nchini ili kuvutia wawekezaji wazawa na wageni na kuwataka kuchangamkia fursa za uwekezaji katika Sekta ya Viwanda yanayotumia madini ya viwandani kama kaolin, dolomite, fieldspar, limestone na mengine yanayopatikana kwa wingi mkoani Tanga.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals