[Latest Updates]: Nyongo aitaka Tume ya Madini kuchunguza chanzo cha mgogoro wa wachimbaji madini, Kilwa

Tarehe : Dec. 17, 2018, 10:10 a.m.
left

Na Greyson Mwase, Kilwa

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameitaka Tume ya Madini kufanya uchunguzi kuhusu mgogoro kati ya kampuni inayojihusisha na uchimbaji wa madini ya jasi ya Kizimbani inayomilikiwa na Seleman Mohamed na wananchi wa kijiji cha Hotel Tatu kilichopo Wilayani Kilwa mkoani Lindi.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya wazalishaji wa madini ya chumvi mara baada ya kumalizika kwa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.[/caption]

Naibu Waziri Nyongo ametoa agizo hilo leo tarehe 15 Desemba, 2018 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho wakati wa utatuzi wa mgogoro huo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa wa Lindi yenye lengo la kukagua shughuli za madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Alisema kuwa, baada ya kusikiliza pande zote mbili imeonekana kuna haja ya  Tume ya Madini kufanya uchunguzi ili kubaini namna utoaji wa leseni ya uchimbaji wa madini ya jasi kwa kampuni ya Kizimbani ulivyofanyika kabla ya kufanya maamuzi kwa mujibu wa sheria na kanuni za madini.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Nyongo alisisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini haitasita kuwaondoa maafisa madini wakazi wa mikoa watakaobainika kuwa ndio chanzo cha migogoro kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini.

“Kama Serikali tunataka kuhakikisha leseni za utafiti na uchimbaji wa madini zinatolewa kwa kufuata sheria na kanuni za madini bila kuwepo kwa migogoro ya aina yoyote, aidha hatutasita kumwondoa afisa madini mkazi yeyote atakayebainika kuwa chanzo cha migogoro kwenye shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini,” alisema Naibu Waziri Nyongo huku akishangiliwa na wananchi.

Awali wakielezea mgogoro huo kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema kuwa walikuwa na mgogoro wa muda mrefu kati yao na Seleman Mohamed aliyedai kuwa mmiliki halali wa eneo husika hali iliyopelekea mgogoro kuwasilishwa kwenye Ofisi ya Madini Mtwara, ambapo  mtaalam kutoka ofisi hiyo alifika kwa ajili ya kuchukua alama za eneo husika kwa ajili ya kwenda kuhakiki umiliki wa eneo husika.

Waliendelea kusema kuwa, walifika katika Ofisi hiyo baada ya siku mbili na kuelezwa kuwa eneo hilo lilishaombewa leseni na kutolewa kwa mmiliki wa kampuni ya Kizimbani, Seleman Mohamed.

Walisema kuwa tangu kuzuka kwa mgogoro huo mwaka 2013, wamekwenda katika ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Mkoa pasipo mafanikio yoyote na kusisitiza kuwa wanahitaji eneo hilo kwa ajili ya uwekezaji kwenye shughuli za uchimbaji wa madini ya jasi kwa kutumia mwekezaji na  kujipatia kipato pamoja na kulipa kodi Serikalini.

Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Hoteli Tatu kilichopo Wilayani Kilwa Mkoani Lindi wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) wakati wa mkutano wa utatuzi wa mgogoro baina ya kijiji hicho na mmiliki wa kampuni inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya jasi ya Kizimbani, Seleman Mohamed.[/caption]

Kwa upande wake mmiliki wa leseni hiyo, Seleman Mohamed alidai kuwa aliomba leseni kwa kufuata sheria na kanuni za madini na kupatiwa leseni yake.

Wakati huo huo akizungumza katika nyakati tofauti kupitia mikutano na wazalishaji wa chumvi iliyofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi na katika eneo la Kilwa Masoko Wilayani Kilwa mkoani Lindi, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini inatambua mchango wa wazalishaji wa chumvi hususan katika mkoa wa Lindi kwenye Sekta ya Madini hivyo imeweka mikakati mbalimbali ya kuwasaidia.

Alieleza mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuondoa tozo mbalimbali tisa kisheria zilizokuwa zinatozwa na halmashauri ili uzalishaji wao uwe na tija na kuinua uchumi wa mkoa wa Lindi.

Alieleza kuwa mikakati mingine kuwa, ni pamoja na kuendelea kushughulikia changamoto zilizopo kwenye uzalishaji chumvi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha chumvi katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi mara baada ya kupata eneo na fedha kutoka Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini. (SMMRP) uliopo chini ya Wizara ya Madini.

Aliendelea kusema kuwa mahitaji ya chumvi nchini ni takribani tani laki tatu na nusu kwa mwaka ambapo asilimia 70 ya chumvi inaagizwa kutoka nje ya nchi  na kusisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imejipanga katika uboreshaji wa uzalishaji wa chumvi nchini.

“Kama Wizara ya Madini tunataka ifike mahali tuzalishe chumvi bora ya kutosha na kuuza ya ziada nje ya nchi na kujiingizia fedha za kigeni,” alisema Naibu Waziri Nyongo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Nyongo aliwataka wazalishaji wa chumvi hao kufuata sheria na kanuni za madini.

Wakizungumza katika nyakati tofauti wazalishaji wa chumvi mkoani Lindi waliwasilisha changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na tozo zilizoondolewa kisheria kwenye madini ya chumvi kuendelea kutozwa na halmashauri, ukosefu wa mitaji pamoja na masoko.

Changamoto nyingine ni pamoja na miundombinu duni kwenye maeneo yenye uzalishaji wa chumvi, madini joto yanayotumika kwenye uzalishaji wa chumvi kuuzwa kwa gharama kubwa na kutotambuliwa katika halmashauri na taasisi  nyingine za kifedha.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals