Tarehe : April 28, 2018, 12:29 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameuagiza Uongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), kuanza mara moja mchakato wa kuwalipa fidia wananchi wa Mtaa wa Nyamalembo mjini Geita, ambao nyumba zao zimeathiriwa na milipuko inayofanywa na Mgodi huo.
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (katikati) akisaidia kuponda mawe katika eneo la Mradi wa uchenjuaji dhahabu, kijiji cha Nyakabale, wilayani Geita wakati alipotembelea eneo hilo, akiwa katika ziara ya kazi, Februari 24 mwaka huu.[/caption]
Aidha, Naibu Waziri ameutaka Mgodi huo kuchagua moja kati ya kuwalipa fidia wananchi wa Kijiji cha Nyakabale ambacho kipo ndani ya eneo la Leseni yao, ili waondoke au kutoa tamko la kuwaruhusu kuendelea na shughuli mbalimbali za kimaendeleo katika eneo hilo.
Nyongo ametoa maagizo hayo Februari 23 na 24 mwaka huu, akiwa katika ziara ya kazi mkoani Geita, ambapo alikutana na wananchi wa maeneo husika kujionea hali halisi, kuzungumza nao na kisha kukutana na uongozi wa GGM.
“Naagiza, kuanzia Jumatatu Februari 26, ninyi GGM kwa kushirikiana na Timu iliyofanya uthamini wa nyumba zilizoathiriwa pamoja na ile Timu ya Serikali, mkae pamoja kuandaa mchakato wa kuwalipa wananchi hawa. Suala hilo nitalisimamia ili kuhakikisha wote ambao nyumba zao zimeathiriwa wanapatiwa fidia.”
Nyongo alisema anatambua kuwa GGM wanatumia kigezo cha sheria na kanuni inayowaruhusu kutolipa fidia ya ardhi katika maeneo ambayo bado hawajaanza kuyafanyia kazi, lakini hata hivyo aliwataka kutumia kigezo cha ubinadamu na uhusiano mwema kuwalipa wananchi hao.
Alitahadharisha kwamba, yawezekana kukawa na udhaifu au upungufu katika sheria na kanuni mbalimbali zinazoongoza sekta husika, na kwamba wako baadhi ya watu wanaotumia mwanya huo kuwakandamiza wengine, hususan wananchi.
“Sasa kama kuna sheria na kanuni zinazombana mwananchi, tuko tayari kuzirekebisha. Hata hivyo, nawaasa, msitumie udhaifu wa sheria kumkandamiza mwananchi wa kawaida.”
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyakabale – Geita, wakati wa ziara yake ya kazi, Februari 24 mwaka huu.[/caption]
Naibu Waziri Nyongo alisema Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi makini wa Rais John Magufuli, haiwezi kukubali kuona mwekezaji yeyote anakuwa kero kwa wananchi.
“Hatuko tayari kumwona mwananchi anaonewa na mwekezaji. Tunataka watu waishi kwa amani, wafurahie uwekezaji ambao tumeukaribisha. Hatutasita kukuchukulia hatua wewe ambaye unatumia udhaifu wa sheria kumwonea mwananchi.”
Akizungumzia umuhimu wa kujenga uhusiano mzuri na amani ya kudumu baina ya wawekezaji na jamii inayowazunguka, Nyongo alisema kuwa suala hilo linawezekana endapo kutakuwa na utaratibu wa mazungumzo na makubaliano ya masuala mbalimbali kati ya pande zote husika.
Hata hivyo, Naibu Waziri alibainisha kuwa lengo la Serikali siyo kuwafukuza wawekezaji bali ni kuhakikisha wanafanya kazi yao ya uwekezaji pasipo kuwakandamiza wananchi.
Alisema kuwa, ni lazima pande zote mbili zihakikishe zinafuata sheria na taratibu zilizowekwa, lakini wasisahau kujenga mahusiano mazuri baina yao.
Akizungumzia tabia ya baadhi ya wachimbaji wadogo kuvamia maeneo ya leseni za wawekezaji wakubwa, Nyongo alisema kuwa siyo sahihi na kuwataka kuacha mara moja kwani ni kinyume cha sheria.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Nyakabale, Wilaya ya Geita wakiwasilisha maoni yao kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), wakati wa ziara yake ya kazi hivi karibuni.[/caption]
“Wako wanaopotosha kauli na agizo la Mheshimiwa Rais wetu, aliposema kuwa wachimbaji wadogo walio katika maeneo yao wasibugudhiwe bali waachwe waendelee na kazi yao ya uchimbaji katika maeneo hayo. Naomba ieleweke kuwa, Mheshimiwa Rais hakusema mwende mkavamie leseni za wawekezaji bali mbaki katika maeneo yenu, na yeyote asiwaondoe.”
Akifafanua zaidi, alisema kuwa, Serikali imeanzisha Kamisheni maalum itakayoshughulikia sekta ya madini, na kwamba inatarajiwa kuanza kufanya kazi hivi karibuni. Aliwataka wachimbaji wadogo wasio na leseni wahakikishe wanafuata taratibu husika mara tu Kamisheni hiyo itakapoanza kufanya kazi ili wapate leseni na kurasimishwa katika kazi hiyo.
Alisema kuwa, Serikali inataka kuona wachimbaji wote wa madini wanafanya kazi zao kwa amani ili walipe kodi na tozo zote stahiki ili kuwezesha kuongeza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri aliuagiza Mgodi wa GGM kuzingatia umuhimu wa kuwawezesha wananchi wanaowazunguka na Taifa kwa ujumla kwa kutumia na kutoa kipaumbele kwa bidhaa na huduma zinazopatikana ndani ya nchi na maeneo ya jirani kwani suala hilo lipo kisheria.
Awali, akizungumza katika ziara hiyo, Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Ziwa Viktoria – Magharibi, Mhandisi Yahya Samamba alisema mgogoro husika umekuwa wa muda mrefu hivyo ni wakati muafaka hatua stahiki zikakamilishwa ili kurejesha amani katika eneo hilo.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Nyakabale, Wilaya ya Geita wakiwasilisha maoni yao kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), wakati wa ziara yake ya kazi hivi karibuni.[/caption]
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Herman Kapufi pamoja na kupongeza maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia uwazi, upendo na utashi kwa pande zote mbili ili kuhakikisha kunakuwa na suluhisho la kudumu la migogoro husika.
Mbunge wa Geita Mjini, Costantine Kanyasu, aliishukuru Serikali kwa dhamira ya dhati iliyoonesha ya kushughulikia migogoro hiyo ambayo alisema imekuwa ikiwasononesha wananchi wa Geita kwa muda mrefu.
Imeandaliwa na:
Veronica Simba, Geita
Afisa Habari,
Wizara ya Madini,
5 Barabara ya Samora Machel,
S.L.P 2000,
11474 Dar es Salaam,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,
Barua Pepe: info@madini.go.tz,
Tovuti: madini.go.tz
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.