Tarehe : May 7, 2018, 9:57 a.m.
Waziri wa Madini Angellah Kairuki amekabidhi vitendea kazi mbalimbali vyenye thamani ya jumla ya Dola za Marekani 350,000 kwa Ofisi za Madini za Kanda mbalimbali nchini.
Waziri wa Madini Angellah Kairuki (kushoto) akikabidhi vitendea kazi mbalimbali kwa baadhi ya Makamishna Wasaidizi wa Madini wa Kanda, Makao Makuu ya Wizara Dodoma, Mei 4 mwaka huu.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa Makamishna Wasaidizi wa Madini wa Kanda hizo, jana Mei 4 2018 Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma; Waziri Kairuki aliwataka wahusika kuvitunza kutokana na gharama kubwa iliyotumika kuvinunua.
“Serikali imekopa kwa ajili ya kuhakikisha sekta ya madini inaendelezwa ili iweze kuchangia zaidi katika uchumi wa nchi. Tunaamini vitawasaidia sana katika utendaji wa majukumu yenu. Mvitunze.”
Akifafanua kuhusu vifaa vilivyotolewa, Waziri alisema kuwa ni pamoja na kifaa maalum kinachotumia teknolojia ya kisasa kung’amua uwepo wa aina ya gesi hatarishi kwa afya, chini ya Migodi ya Madini.
Alisema kuwa kifaa hicho kinamsaidia muhusika kutambua sehemu yenye hewa hiyo hatarishi na hivyo kuchukua hatua stahiki za kujiepusha na ajali inayotokana na kuvuta hewa ya aina hiyo.
Aidha, alitaja vifaa vingine kuwa ni kifaa maalum cha kukuza taswira za madini kinachojulikana kitaalam kama ‘Hand Lens’. “Kifaa hiki hutumika katika shughuli za uthaminishaji madini ya vito ambapo husaidia kuyakuza madini husika katika ukubwa unaotakiwa ili kukokotoa thamani yake halisi tofauti na unapotumia macho ya kawaida,” alifafanua.
Vingine ni pamoja na GPS zinazotumika kupima mipaka ya maeneo, ‘Printer’, viatu na sare maalum vinavyotumika migodini, Kompyuta, na vifaa vingine vya kijiolojia.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini ambaye pia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini, Prof. Shukrani Manya alisema kuwa vifaa hivyo vimetolewa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali za Madini (SMMRP).
Alisema kuwa, zoezi la kugawa vifaa hivyo limefanyika katika awamu kadhaa, ambapo kwa awamu ya kwanza, Kanda za Madini zilizogawiwa ni Kanda ya Kusini (Mtwara na Nachingwea), Kanda ya Ziwa Nyasa (Songea, Njombe na Tunduru), Kanda ya Kusini Magharibi (Chunya) na Makao Makuu ya Wizara (Ofisi ya Ukaguzi wa Migodi, wachimbaji wadogo na utoaji leseni).
Nyingine ni Ofisi za Madini za Singida, Dodoma, Morogoro, Tanga, Handeni, Musoma, Bariadi, Mpanda, Kigoma, Mwanza, Geita, Bukoba, Arusha, Moshi, Mirerani na Tabora.
“Vifaa vilivyobaki ni kwa ajili ya Ofisi za Shinyanga, Kahama, Kituo cha Uongezaji Thamani Madini (TGC), Ofisi ya Biashara ya Madini na Ofisi ya Kamishna wa Madini, ambao ndiyo wanaopatiwa leo hii,” alifafanua Prof. Manya.
Akizungumza baada ya zoezi hilo la kukabidhi vifaa; Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof Idris Kikula alisema kuwa, ni jambo la kutia faraja kwa kupata vitendea kazi kwa Ofisi hizo za Madini, ambazo kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria ya Madini yaliyofanyika mwaka 2017, sasa ziko chini ya Tume.
Alisema kuwa, upatikanaji wa vifaa hivyo vya kisasa utasaidia Tume kutimiza jukumu lake kubwa la kusimamia mapato stahiki ya Taifa yanayotokana na shughuli za madini.
Imeandaliwa na:
Veronica Simba, Dodoma
Afisa Habari,
Wizara ya Madini,
Kikuyu Avenue,
P.O Box 422,
40474 Dodoma,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,
BaruaPepe: info@madini.go.tz,
Tovuti: madini.go.tz
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.