[Latest Updates]: Prof. Msanjila aongoza wadau kujadili rasimu Kanuni Uanzishwaji wa Masoko ya Madini nchini

Tarehe : Feb. 26, 2019, 1:57 p.m.
left

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila ameongoza kikao kilicholenga kupokea maoni juu rasimu ya kanuni za uanzishwaji wa masoko ya madini nchini.

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa wizara kimewakutanisha, Makamishna Wasaidizi wa Wizara, Rais wa Shirikisho la Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) John Bina, viongozi wa shirikisho hilo pamoja na wawakilishi wa wachimbaji wadogo kutoka mikoa ya kimadini nchini.

Akizungumza wakati wa Ufunguzi wa kikao, Prof. Msanjila alisema maoni ya wajumbe hao ni muhimu kwa watanzania na taifa kwa ujumla katika kuboresha kanuni hizo.

Aidha, Msanjila amebainisha kuwa, wadau wengine wamekwisha kutoa maoni yao katika makundi tofauti tofauti na pia maoni mengine yanaendelea kupokelewa kwa njia ya maandishi na kuwataka maoni hayo yakamilishwe ndani ya kipindi cha wiki moja.

Kabla ya kupokea maoni hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Sheria wa Wizara, Edwin Igenge aliwasilisha rasimu ya kanuni hizo ili kutoa uelewa wa kile wanachopaswa kuchangia katika kutoa maoni yao.

Akiwasilisha rasimu hiyo, Igenge alisema hii ni sheria ndogo inayotokana na sheria mama ya madini. “Kanuni hizo zinatungwa kwa mujibu wa kifungu cha 27 (C) kifungu kidogo cha pili pamoja na kifungu cha 129 cha sheria ya madini,” amesema Igenge.

Aidha, amesema mahala patakapo kuwa na soko la madini kutakuwa na huduma zote zinazotakiwa ili kurahisisha ubadilishwaji wa fedha na  madini kama vile mabenki, ofisi za mamlaka ya Mapato (TRA), ofisi za masuala ya ulinzi na usalama, pamoja na ofisi mbalimbali za serikali.

Igenge amesema baada ya kukamilika na kupitishwa kwa kanuni hizo zitatafsiriwa na kupatikana katika lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi wote kuelewa kanuni na mwongozo wa masoko ya madini.

Akizungumzia baadhi ya vipengele vilivyopo katika rasimu hiyo, Igenge alisema sehemu ya kwanza inahusika na utangulizi yenye vifungu 3 cha kwanza ni jina la kanuni ambapo litaitwa ‘Kanuni za masoko za mwaka 2019’, pili ni maelezo ya wapi kanuni hizo zitatumika na kuratibiwa na kipengele cha mwisho kitatoa tafsiri ya maneno mbalimbali yanayotumika ndani ya kanuni hizo.

Sehemu ya pili ya kanuni inahusika na uanzishwaji wa masoko yenyewe, ambapo masoko yataanzishwa katika maeneo yenye tawala za mikoa na kuipa maelekezo Tume ya Madini kuhakikisha wanashirikiana na tawala za mikoa katika kuanzisha masoko hayo.

Aidha, alielezea msingi wa kwanza ni msingi wa uwazi, msingi wa matangazo ili watu waweze kujua madini yanauzwa na kununuliwa wapi, msingi wa haki ambao utazuia manunuzi haramu ya madini, lakini pia msingi wa mwendelezo ikiwa na maana masoko hayo kuwa ni masoko ya kudumu na si ya msimu.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, ameiomba serikali kuyafanyia kazi maoni yaliyotolewa na wawakilishi wa wachimbaji wadogo ili kupata kitu kitakachokubalika na jamii nzima ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini.

Aidha, alikiri kufurahishwa na ufafanuzi uliotolewa katika kila kipengele cha rasimu ya kanuni za uanzishwaji wa masoko ya madini na kukiri kwamba wanaamini kuwa serikali ina nia njema na wananchi wake.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals