[Latest Updates]: Wizaya ya Madini Yatoa Semina kwa Kamati ya Bunge

Tarehe : Sept. 14, 2022, 9:11 a.m.
left

Tume ya Madini yaeleza mikakati ya kutatua tozo za wachimbaji wadogo za Mamlaka nyingine

STAMICO yasema iko mbioni kuanzisha mgodi wake wenyewe*

GST yatakiwa kufanya tafiti kwenye Halmashauri zisizonufaika na mapato ya Madini

Asteria Muhozya na Steven Nyamiti- Dodoma

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa tayari imekwisha kuchukua hatua  kadhaa  za kushughulikia  changamoto ya uwepo wa tozo nyingi zinazotozwa na Taasisi  nyingine za Serikali kwa wachimbaji wadogo wa madini ikilenga kuwezesha shughuli hizo kufanyika kwa tija.

Mhandisi Samamba ameyasema hayo katika warsha ya Siku moja kwa kamati hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Madini kwa lengo la kuijengea uelewa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya madini ikiwemo mwenendo wa sekta na biashara ya madini nchini.

Amesema kuwa,  tayari  Wizara imekwisha kutana na Wizara ya Fedha na Mipango kujadiliana kuhusu utitiri wa tozo kwa wachimbaji wadogo wa madini zinazotozwa na taasisi nyingine  suala ambalo linapelekea kuwepo changamoto kwenye utekelezaji wa shughuli na biashara ya madini.

Pia, ameeleza kuwa, tayari Serikali kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022, imefanya mabadiliko kwenye Sheria ya TASAC na kuongeza kwamba, Tume ya Madini inatarajia kukutana na Ofisi ya  Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)  kujadiliana kuhusu suala la tozo kwa wachimbaji wadogo ikiwemo kukutana na Wakurugenzi wa Halmashauri na wadau wa madini kwa ajili ya ufumbuzi na kutatua changamoto hiyo katika kikao kinachotarajiwa kufanyika  hivi karibuni.

Akizungumzia mwenendo wa hali ya uwekezaji katika Sekta amesema, uwekezaji umeendelea kuongezeka kutokana na juhudi zinazofanywa na wizara za kuvutia uwekezaji na kueleza kwamba, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2022/23 Tume ya Madini imepanga kutoa Leseni 9,172.

Pia, ameileza kamati hiyo kuwa, baada ya kanzishwa kwake mwaka 2017, ilipewa majukumu 22, huku majukumu matatu makuu yakiwa ni ukusanyaji wa maduhuli, usimamizi na utoaji wa leseni,  ukaguzi wa migodi na udhibiti wa biashara  ya madini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse akieleza  hali ya uwekezaji kwa shirika hilo  pamoja na mambo mengine ameeleza kwamba, kwa mara ya kwanza shirika hilo linatarajia kuanzisha mgodi wake mwenyewe katika leseni ya dhahabu ya Kigosi  mkoani Geita na tayari fedha za utekelezaji huo zimetengwa katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/23 ambapo linatarajia kukamilisha utafiti kwa ajili ya maandalizi ya uchimbaji dhahabu.

Akizungumzia  mipango ya  shirika hilo amesema ni pamoja na kuongeza mapato yake ya ndani kwa mwaka huu wa fedha ambapo linatarajia mapato hayo kufikia shilingi bilioni 70 na kuondokana kabisa utegemezi wa  fedha za serikali.

Dkt. Mwasse ameeleza mipango mingine na kuitaja kuwa ni pamoja na kuimarisha shughuli za uchorongaji  kwa kununua mitambo na vifaa vya kisasa zaidi sambamba  na kutafuta kandarasi zaidi za uchorongaji katika migodi mikubwa  ya kati ndani na nje ya nchi.

Pia, ameongeza kuwa  shirika hilo limepanga kuimarisha miradi yake ya uchimbaji wa makaa ya mawe na kuongeza mitambo ya utengenezaji wa Mkaa mbadala (Rafiki Briquettes) utaosambazwa maeneo mbalimbali.

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amewasilisha kwa kamati hiyo Mfumo wa kudhibiti biashara ya Tanzanite ikiwa pia ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu aliyoyatoa  mwaka 2021, wakati akizindua Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery ambapo Rais Samia aliitaka wizara kuongeza thamani ya madini hayo ikiwemo kuhakikisha yanalinufaisha taifa kutokana na upekee wake.

Wakitoa maoni, wajumbe wa kamati wamepongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na wizara ikiwemo taasisi zake  ambapo Mjumbe wa Kamati Mhandisi Stella Manyanya ameishauri  Taasisi ya Jilolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)  kuangalia uwekezano wa kufanya tafiti ambazo zitasaidia kubaini uwepo wa madini  katika halmashauri ambazo hazinufaiki na mapato yanayotokana na shughuli za madini ili kuziwezesha halmashauri hizo kunufaika na rasilimali hiyo kama zilivyo nyingine.

Mbali na kamati hiyo, kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Adolf Ndunguru, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya  Madini Msafiri Mbibo, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula, Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo, Menejimenti ya  Wizara, Wakuu wa Taasisi chini ya Wizara na Wataalam kutoka wizarani na taasisi zake.

 

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals