[Latest Updates]: Biteko akunwa na utendaji kazi wa Mgodi wa Kambas

Tarehe : July 20, 2018, 4:51 a.m.
left

  • Ataka migodi mingine nchini kuiga mgodi huo

Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko amepongeza utendaji kazi wa mgodi wa kuzalisha makaa ya mawe wa Kambas uliopo wilayani Songea mkoani Ruvuma na kuitaka migodi mingine nchini kuiga mfano kwenye uchimbaji madini kutoka  kampuni hiyo.

Mtendaji Mkuu wa Mgodi wa Kuzalisha Makaa ya Mawe wa Kambas, Yahya Yusuph Kambaulaya (katikati) akielezea shughuli za kampuni hiyo kwa Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko ( wa pili kushoto mbele) kwenye ziara yake katika mgodi huo uliopo katika kijiji cha Maniamba kilichopo Songea mkoani Ruvuma. Kushoto kabisa mbele ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme.

Biteko ameyasema hayo leo  tarehe 17 Julai, 2018 kwenye ziara yake aliyoifanya katika mgodi huo uliopo katika kijiji cha  Maniamba wilayani Songea mkoani Ruvuma, lengo likiwa ni kukagua shughuli za uchimbaji madini katika mgodi huo pamoja na kutatua changamoto zilizopo.

Katika msafara wake aliambatana na wataalam kutoka Wizara ya Madini, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme, Maafisa Madini wa Songea, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema pamoja na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya ya Songea.

Mara baada ya kupokea taarifa ya shughuli za uchimbaji madini katika mgodi huo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mgodi huo, Yahya Yusuph Kambaulaya, Naibu Waziri Biteko aliuopongeza mgodi huo kwa kuweza kuzalisha makaa ya mawe na kuuza ndani ya kipindi kifupi tangu imeanza uchimbaji wake Desemba mwaka 2017.

Aidha, aliutaka mgodi huo kuunganisha leseni zake 14 za madini  ili kuweza kuwa wachimbaji wa kati hatimaye kuwa wachimbaji wakubwa na kuzidi kuongeza mapato Serikalini.

“Kampuni hii imeanza baada ya Sheria Mpya ya Madini ya mwaka 2017 ambayo ni rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, ndani ya kipindi kifupi wameanza kuchimba kwa mafanikio makubwa, kutoa ajira kwa wazawa na kushiriki katika shughuli za huduma za jamii ( corporate social responsibility), nazitaka kampuni za madini  zote nchini kuiga mfano wa kampuni hii,” alisema Biteko.

Aliendelea kusema kuwa,  ni matarajio yake kuona mgodi wa Kambas unazidi kukua na kuitaka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,  Halmashauri ya Songea, na Afisa Madini kuulea mgodi huo  huku wakihakikisha unafuata  sheria na kanuni za madini.

Shughuli za uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe zikiendelea katika Mgodi wa Kambas.

Aidha Biteko alitaka halmashauri kutumia fedha inazopata kama mapato kwenye mgodi huo kwenye uwekezaji mwingine mbadala kama vile shule, vituo vya afya na barabara ili kuacha kumbukumbu nzuri katika vizazi vijavyo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko aliutaka mgodi wa Kambas kulipa kodi stahiki serikalini mara baada ya kufanyika kwa mauzo kwenye kituo cha mwisho (gross value) badala ya mauzo ya hapo hapo mgodini (net back value).

“Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kifungu cha 87 (6) kinaeleza kuwa kodi ya madini itakokotolewa baada ya bei ya mwisho nje ya nchi kule yanapouzwa madini hayo na si hapa mgodini, hivyo ninaona ni vyema niwaambie mapema ili kusijitokeze kasoro baadaye,” alisisitiza Biteko.

Aidha, Biteko aliwataka wananchi walioajiriwa  katika mgodi wa Kambas kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kutoa ushirikiano kwa mwekezaji huyo mwenye nia ya dhati ya kuwasaidia wananchi hao.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mdeme mbali na kumpongeza Naibu Waziri Biteko kwa usimamizi makini wa  sekta ya madini nchini aliongeza kuwa, ofisi yake ipo tayari kushirikiana na mwekezaji huyo pamoja na kutatua changamoto zitakazojitokeza.

Awali, akiwasilisha taarifa ya uzalishaji, Mtendaji Mkuu wa Mgodi wa Kuzalisha Makaa ya Mawe wa Kambas, Yahya Yusuph Kambaulaya alisema kuwa uzalishaji wa makaa ya mawe katika mgodi huo umekuwa ukiongezeka siku hadi siku ambapo mpaka sasa wameshachimba tani 5138.

Mtendaji Mkuu wa Mgodi wa Kuzalisha Makaa ya Mawe wa Kambas, Yahya Yusuph Kambaulaya (katikati) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (wa pili kushoto). Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme.

Alifafanua kuwa tani hizo zilichimbwa kwa muda wa miezi mitatu ya Desemba 2017, Mei, 2018 na Juni, 2018 na kuendelea kufafanua kuwa kati ya kipindi cha Januari hadi Aprili, 2018 shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe zilisimama kutokana na mvua kubwa.

Aliendelea kusema kuwa, kuanzia Julai 2018 uzalishaji wa makaa ya mawe kwa siku ni tani 200 na kusisitiza kuwa malengo ya mgodi ni kuzalisha  tani 600 hadi 700 kwa siku ambapo kwa mwezi mgodi utakuwa na uwezo wa kuzalisha kati ya tani 18,000 hadi 21,000.

Akielezea manufaa ya mgodi wa Kambas, Kambaulaya alisema mgodi umeweza kulipa serikalini kodi mbalimbali inayotokana na mauzo ya makaa ikiwa ni pamoja na mrabaha na ada ya ukaguzi  shilingi milioni 16,  shilingi milioni 4.1 katika kijiji cha Maniamba kama mchango kwa huduma za jamii.

Alisema pia mgodi wake ulichangia katika huduma za kijamii katika ujenzi wa Shule ya Msingi Mipeta iliyoezuliwa paa na upepo mwezi Desemba, 2017 kwa kutoa vifaa vya viwandani vyenye thamani ya shilingi milioni tano na ukarabati wa ofisi ya kijiji cha Maniamba kupitia vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya shilingi milioni nne.

Kambaulaya aliendelea kusema kuwa mgodi wa Kambas pia umefanikiwa kutoa ajira 20 rasmi na zisizo rasmi 50 hivyo kukuza uchumi wa wananchi wanaozunguka mgodi.

Akielezea maratajio ya mgodi wa Kambas, Kambaulaya alisema mgodi unatarajia kupanuka zaidi kwa kuanzisha mchakato wa uzalishaji wa umeme unaotokana na makaa ya mawe kwa kushirikiana na kampuni ya BBIC kutoka Chini ambapo mpaka sasa wameshasaini makubaliano ya awali ya namna ya kujenga mtambo  wa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe wenye uwezo wa Megawati 500 hadi 1000 ambapo  umeme huo utaingizwa kwenye Gridi ya Taifa.

Aidha, akielezea changamoto za mgodi huo Kambaulaya alieleza kuwa ni pamoja na miundombinu ya barabara kutokuwa rafiki katika usafirishaji wa makaa ya mawe na kutafuta njia sahihi ya kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe kulingana na tabaka la makaa yanayopatikana katika eneo hilo.

Imeandaliwa na:

Greyson Mwase, Songea

Afisa Habari,

Wizara ya Madini,

Kikuyu Avenue,

P.O Box 422,

40474 Dodoma,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

BaruaPepe: info@madini.go.tz,                                             

Tovuti: madini.go.tz

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals