[Latest Updates]: Wanajiosayansi waaswa kutathmini mchango wao katika Tanzania ya viwanda

Tarehe : Oct. 1, 2018, 7:55 a.m.
left

Nuru Mwasampeta na Samwel Mtuwa, Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewaasa Wanajiosayansi kutathmini mchango wao katika maendeleo ya nchi, hususan katika maendeleo ya Tanzania ya Viwanda.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa wito huo tarehe 27/09/2018 alipokuwa akifungua Warsha ya siku Nne ya Wataalamu wa jiolojia iliyofanyika katika hoteli ya Dodoma jijini Dodoma yenye lengo la kutathmini mchango wa wanajiosayansi katika maendeleo ya viwanda nchini.

Mkutano huo pia unalenga katika kuwaleta pamoja wataalamu hao ili kujadili masuala mbalimbali ya sayansi ya dunia na umuhimu wake kwa jamii.

Akizungumzia umuhimu wa tasnia hiyo, Majaliwa alisema jiolojia ni sayansi inayogusa kila nyanja ya maisha ya binadamu ikiwemo kilimo kitokanacho na udongo utokanao na miamba, maji yapatikanayo ardhini, metali mbalimbali zipatikanazo ardhini kwa ajili ya matumizi katika viwanda ikiwa ni pamoja na vyanzo vya nishati vinavyohusiana moja kwa moja na jiolojia kama vile joto ardhi, makaa yam awe, mafuta na gesi na madini kama vile urani.

Kutokana na umuhimu huo mkubwa wa jiolojia Majaliwa amewataka watanzania kuendelea kutafuta utaalamu huo ili waweze kuchangia katika kuharakisha maendeleo ya nchi yetu.

“Nchi yetu imebarikiwa kuwa na rasilimali za asili nyingi kama vile madini, vito, mafuta gesi asilia, makaa ya mawe . Tanzania ni moja ya nchi chache duniani zilizobarikiwa kuwa na rasilimali hizi kwa wingi hivyo kupelekea kila majadiliano ya mali asili duniani Tanzania kutajwa pia,” alisisitiza.`

Aliongeza kuwa, kutokana na baraka ambazo nchi imejaliwa na Mwenyezi Mungu, nchi inanufaika kutoka na michango mikubwa miwili ya jiosayansi ya kwanza ikiwa ni mchango wake katika sekta ya viwanda, ambapo ili kuweza kufikia Tanzania ya Viwanda tunahitaji malighafi zizalishwe kwa wingi ili zitumike katika viwanda vinavyoanzishwa nchini.

Akizitaja malighafi hizo, Majaliwa  alisema ni kama vile madini ya  kinywe (graphite), jasi, chokaa, kaolini madini ambayo yanahitajika kwa wingikatika kuchochea uzalishaji wa bidhaa za viwandani.

Aidha, Majaliwa aliwataka wanajiolojia kuhakikisha kuwa  wanaonesha ni wapi madini hayo yanapatikana ili kuwawezesha watanzania na wawekezaji kuweza kuyapata na kuyatumia katika viwanda vyao. “Mnatakiwa mtuambie yako wapi na yana kiwango gani ili wazalishaji wa bidhaa za viwandani waweze kupata malighafi hizi kwa urahisi ili kuongeza tija katika viwanda vyetu hapa nchini.” Majaliwa alisisitiza.

Akizungumzia mchango wa pili mkubwa wa jiosayansi, Majaliwa alisema ni katika upatikanaji wa maji ya kutosha nchini. Alieleza kuwa ili kuwa na viwanda vinavyozalisha kwa ufasaha nchini maji lazima yawepo kwani ni bidhaa muhimu katika kuchangia maendeleo ya viwanda nchini.

Majaliwa alitanabahisha kuwa jukumu la wanajiolojia nchini ni kuonesha ni wapi maji yanapatikana ardhini kutokana na ukweli kuwa maji ya ardhini ni mara 5,000 ya maji yanayopatikana katika uso wa dunia.

Kwa kuzingatia kuwa maji yanapatikana popote ardhini aliwataka wataalamu hao kuandaa utaratibu utakaowezesha kuwa na takwimu za uhakika kuhusu kiwango cha maji, mahali yalipo na ujazo wake ili kuweza kuvutia uwekezaji wa viwanda kote nchini.

Aidha, alibainisha mchango mwingine mkubwa wa jiosayansi kuwa ni katika masuala ya nishati ambapo tutapata mchango kutokana na joto ardhi, rasilimali za gesi asilia ambapo gesi asilia pia imeshaanza kutumika katika viwanda vyetu nchini. Alisema, tafiti bado zinahitajika ili ufumbuzi uendelee na gesi yakutosha iweze kugunduliwa ili kutosheleza mahitaji ya sasa na baadaye ili kufikia malengo hayo na kueleza kuwa, jukumu hilo linawahusu wanajiolojia.

Akihitimisha hotuba yake ya ufunguzi, Majaliwa aliwataka wanajiolojia hao kujihoji endapo wanajua jukumu lao katika uboreshaji wa sekta ya madini, na endapo wao ni sehemu ya mabadiliko hayo. “Ni matarajio yangu kuwa kwa kushirikiana na Serikali ambayo tayari imejiimarisha Kisera na kimkakati ili kufikia azma ya viwanda, itakayokuwa tayari kuonesha uzalendo wenu na kuhakikisha mchango wenu katika hili unaonekana,” alisema Waziri Mkuu.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Angelleh Kairuki alikiri kwamba wizara  yake iko tayari kutoa ushirikiano kwa wanajiolojia ikiwa ni pamoja na kupokea ushauri wa namna bora ya kuendesha na kuendeleza shughuli za madini nchini.

Aidha, Kairuki alibainisha kuwa wizara inakusudia na itakuwa mstari wa mbele  katika kuanzisha chombo maalumu cha usajili wa Wahandisi  ili kuondoa malalamiko ya watu yanayotokana na baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu kwa kujifanya ni wataalamu wa miamba na ukweli ikiwa sivyo.

Wizara ya madini kupitia taasisi zake itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wanapokea mapendekezo yote yanayotolewa na wataalamu mbalimbali kuhusiana na namna bora ya uendeshaji sekta ya madini hapa nchini na kuyafanyia kazi.

Kutokana na fursa kubwa inayopatikana  katika  sekta ya madini, Kairuki aliwaasa wanajiosayansi kujikita kwenye uwekezaji unaoendana na taaluma yao kutokana na uwepo mkubwa wa rasilimali madini nchini ambayo bado hazijaendelezwa na hivyo kuongeza ufanisi na uwezo wa kiuchumi kwa wanajumuiya hiyo.

Zaidi ya hapo, Waziri Kairuki, alieleza kuwa wizara yake ipo katika mchakato wa kuiwezesha GST kuwa na uwezo wa kukusnya taarifa za kina ambazo zitabaini akiba ya mashapo ya madini mbalimbali yaliyopo nchini.

Uwepo wa taarifa hizo utasaidia kuwavuta na kuwarahisishia wawekezaji pindi wanapotafuta maeneo ya utafiti ili wapate leseni kwenye maeneo ambayo yana taarifa na takwimu za uhakika.

Alibainisha kuwa kasi hiyo itakwenda sambamba na kupitia upya Sera ya madini ya Mwaka 2009 ili iweze kuendana na Marekebisho ya sheria ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 pamoja na kanuni zake za mwaka 2018.

Warsha hii ya wanajiosayansi yenye kauli mbiu isemayo “ Jukumu la wanajiosayansi katika kuendeleza sekta ya viwanda” kwa mwaka huu, hufanyika kila mwaka mara moja.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals