[Latest Updates]: Wachimbaji wa Madini Watakiwa Kuzingatia Usalama Migodini

Tarehe : July 2, 2025, 11:55 a.m.
left

Bariadi, Julai 2, 2025

Tume ya Madini imewataka wachimbaji wadogo wa madini kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na miongozo ya usalama inayotolewa na wataalam wa sekta hiyo ili kukomesha ajali zinazoendelea kuripotiwa katika maeneo ya uchimbaji.

Wito huo umetolewa leo na Kamishna wa Tume ya Madini, Mhandisi Theonestina Mwasha, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usalama kwa wachimbaji wadogo wa madini na wadau wa sekta ya madini kutoka mikoa ya Simiyu na Mara yaliyofanyika mjini Bariadi, mkoani Simiyu.

Mhandisi Mwasha amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini imejipanga kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia elimu, vifaa na teknolojia ili kuwawezesha kujiinua kutoka katika uchimbaji wa kiwango cha chini hadi kuwa wachimbaji wa kati na baadaye wakubwa.

“Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwaongezea uwezo wa kitaalam ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta hii, hususan katika maeneo ya usalama migodini,” amesema Kamishna Mwasha.

Aidha, amewataka wachimbaji hao kuzingatia matumizi salama ya kemikali, hususan zebaki, kwa kuwa matumizi mabaya yake yamesababisha madhara yasiyorekebishika kwa afya ya binadamu na mazingira.

“Mafunzo haya yamejikita katika sheria na kanuni za usalama mahali pa kazi pamoja na Sheria ya Madini. Ni muhimu sana kuhakikisha mnafuata miongozo hii katika kutekeleza shughuli zenu,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkaguzi Mkuu wa Migodi kutoka Tume ya Madini, Mhandisi Hamis Kamando, amesema ajali nyingi zinazotokea migodini husababishwa na kutokuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na mamlaka husika.

Amebainisha kuwa baadhi ya ajali hizo zimesababisha vifo na ulemavu kwa wachimbaji, ambapo changamoto kubwa ni kuanguka kwa miamba, kuteleza katika ngazi na ukosefu wa hewa safi ndani ya maeneo ya uchimbaji.

“Ni wajibu wa kila msimamizi wa mgodi kuhakikisha hatua zote za kiusalama zinafuatwa kikamilifu ili kuzuia madhara haya,” ameongeza Mhandisi Kamando.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Simiyu, Mashauri Ntizu, ameishukuru Tume ya Madini kwa kuandaa mafunzo hayo na kuyafikisha kwa wachimbaji wa mkoa huo.

“Mafunzo haya ni suluhisho la muda mrefu kwa changamoto zinazowakabili wachimbaji. Kupitia semina hii tumejifunza sheria, kanuni na mbinu bora za kufanya kazi kwa usalama,” amesema Ntizu.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwafikia wachimbaji wadogo katika mikoa mingine nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha mazingira ya uchimbaji na kuimarisha mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals