Tarehe : Nov. 20, 2025, 1:55 p.m.
Mbibo afungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi asisitiza ubunifu, uzalendo
Washiriki Baraza la Wafanyakazi kutembelea Mgodi wa GGM
Makusanyo ya Maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini yaliyokusanya na kuwasilishwa Hazina katika kipindi cha Julai hadi Oktoba 2025 yamefikia zaidi ya shilingi bilioni 430.1, sawa na asilimia 35.85 ya lengo la mwaka wa fedha 2025/26 ikiwa lengo la makusanyo ya mwaka mzima ni shilingi trilioni 1.405,537,268,755.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, wakati akifungua Mkutano wa Kwanza wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2025/26, uliofanyika katika ukumbi wa Gold Crest Hotel jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mbibo amesema Serikali inaendelea kuimarisha mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa kupitia utekelezaji wa vipaumbele Saba vilivyowekwa na wizara.
Amesema miongoni mwa vipaumbele hivyo ni kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli, kuendeleza mnyororo wa thamani wa madini muhimu na mkakati, kurasimisha na kuwaendeleza wachimbaji wadogo, pamoja na kuvutia uwekezaji kwenye tafiti za kina za madini.
Ameeleza vingine ni kuimarisha uendeshaji wa minada na maonesho ya madini ya vito, pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na weledi.
Mbibo amesisitiza kuwa uwepo wa Baraza la Wafanyakazi katika sehemu za kazi ni matakwa ya kisheria, hivyo amehimiza wawakilishi wote wa baraza hilo kutoa maoni na mapendekezo yao kwa uhuru ili kuongeza ufanisi wa utendaji wa wizara.
Pamoja mambo mengine, Mbibo amesema washiriki wote wa Baraza hilo wanatarajia kutembelea mgodi wa Geita Gold Mine uliopo mkoani Geita kwa lengo la kujifunza shughuli zinazofanywa migodi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Joseph Ngulumwa, amempongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eng. Yahya Samamba, kwa hatua mbalimbali zinazolenga kuboresha masilahi ya watumishi. Aidha, ameiomba Serikali kupitia menejimenti ya wizara kuimarisha utaratibu wa kusaidia watumishi wanaohitaji matibabu nje ya nchi.
Naye, Hamis Mwisa, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, ameipongeza Wizara ya Madini kwa kufanikisha mkutano huo muhimu, huku akitoa wito kwa watumishi kushiriki kikamilifu kutoa maoni yatakayoboresha masilahi na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika Wizara ya Madini.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.