[Speech]: TAARIFA YA MHESHIMIWA ANTHONY PETER MAVUNDE (MB.),

Tarehe : April 15, 2026
TAARIFA YA MHESHIMIWA ANTHONY PETER MAVUNDE (MB.), WAZIRI WA MADINI KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 15 APRILI, 2026 Ndugu Waandishi wa Habari! Mabibi na Mabwana! “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” Ndugu wanahabari, Awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu, muweza wa yote kwa kutuwezesha kukutana mahali hapa siku ya leo, tukiwa na afya njema. Ndugu wanahabari, Nipo hapa kutoa taarifa ya mambo muhimu kuhusu uendelezaji wa Sekta ya Madini na mwenendo wa vitendo visivyokubalika kwa mustakabali wa maendeleo chanya ya Sekta ya Madini hapa nchini. Ndugu wanahabari, Serikali kupitia Wizara ya Madini inapenda kuujulisha umma kuwa imeendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uendelezaji wa leseni za madini nchini ambapo imebainika kuwepo kwa ongezeko la utoaji wa leseni za madini nchini, kuna baadhi ya wamiliki wa leseni ambao wamekuwa hawatekelezi wajibu wao wa umiliki wa leseni ikiwa ni pamoja na kutokuziendeleza leseni wanazomiliki ndani ya muda uliotolewa kwa mujibu wa Sheria. Wamiliki hao wamekuwa wanahodhi maeneo; hawalipi ada stahiki za leseni; hawatekelezi masuala ya Ushirikishwaji wa Watanzania kwenye shughuli za madini (Local Content), wala Wajibu wa Makampuni kwa Jamii (Corporate Social Responsibility) vilevile wanashindwa kuthibitisha matumizi ya fedha yaliyofanyika pamoja na vielelezo vya matumizi husika kwenye uendelezaji wa leseni hizo. Ndugu wanahabari, Vitendo vya kuhodhi maeneo vimekuwa vikichangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa vitendo vya uchimbaji madini usio rasmi vinavyotokana na uvamizi wa leseni hizo. Vitendo hivyo havivumiliki na Serikali itaendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria na kufuta leseni zote ambazo zitabainika kuwa na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutokuendelezwa ndani ya muda uliotolewa katika Sheria ya Madini Sura 123. Ndugu wanahabari, Katika kutekeleza hatua hiyo ya Serikali, leo natangaza rasmi kufuta leseni 40 za utafutaji madini ambazo wamiliki wake wameshindwa kuziendeleza licha ya kupewa hati za makosa kutakiwa kurekebisha makosa yaliyobainika. Aidha, naiagiza Tume ya Madini kufuta leseni hizo na kuendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara za leseni na kuchukua hatua stahiki za kufuta leseni zote ambazo zitabainika kutokuendelezwa. Aidha, tarehe 10 Aprili, 2026 Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imetoa hati za makosa kwa leseni nyingine 43 zikikujumuisha leseni 40 za utafutaji madini na leseni tatu (3) za uchimbaji wa kati wa madini. Naielekeza Tume ya Madini kuendelea na zoezi la utoaji wa hati za makosa na endapo wamiliki wake watashindwa kurekebisha makosa ndani ya siku 30, leseni hizo zifutwe ili maeneo hayo yatolewe kwa wawekezaji wengine. Ndugu wanahabari, pamoja na hatua hiyo, Serikali imeendelea pia kufuatilia kwa karibu mwenendo wa matukio ya milipuko ya madini ya dhahabu (gold rush) katika maeneo mbalimbali nchini, na kuchukua hatua stahiki kwa lengo la kulinda usalama, kudumisha utulivu, na kuhakikisha uzingatiaji wa sheria na kanuni za madini. Ni vema ieleweke kuwa, kwa mujibu wa sheria za madini za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, shughuli zozote za uchimbaji madini zinapaswa kufanyika kwa kuzingatia umiliki wa leseni halali. Hivyo basi, vitendo vya watu kukimbilia maeneo yenye taarifa za uwepo wa madini na kuanza uchimbaji bila leseni ni kinyume cha sheria na havitavumiliwa. Serikali imekuwa ikichukua hatua za haraka pindi milipuko ya madini inapojitokeza, ikiwa ni pamoja na: Kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao; Kuzuia migogoro kati ya wachimbaji na wamiliki halali wa leseni; Kulinda mazingira dhidi ya uharibifu unaoweza kusababishwa na uchimbaji holela; Kudhibiti hatari za milipuko ya magonjwa ya kuambukiza zinazoweza kujitokeza katika maeneo ya gold rush. Katika maeneo ya gold rush, mara nyingi hukusanyika watu wengi kwa muda mfupi katika mazingira yasiyo rasmi yenye msongamano mkubwa, hali inayoongeza uwezekano wa kuenea kwa magonjwa ya milipuko. Kutokana na hali hiyo, Serikali huchukua hatua mahsusi za kiafya, ikiwa ni pamoja na: Kuratibu uwepo wa huduma za afya za dharura kwa kushirikiana na mamlaka za afya za maeneo husika; Kuhamasisha na kusimamia usafi wa mazingira, upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na huduma za vyoo; Kutoa elimu ya afya kwa wachimbaji na wadau kuhusu kinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza; Kufuatilia na kudhibiti magonjwa ya mlipuko yanayoweza kujitokeza, ikiwemo magonjwa ya mfumo wa hewa, magonjwa ya mlipuko wa tumbo na mengineyo; Kuchukua hatua za haraka za kinga na tiba pale dalili za mlipuko wa ugonjwa zinapobainika. Ndugu wanahabari, Baada ya hali ya usalama kudhibitiwa, Serikali hufanya tathmini ya eneo husika, na pale inapobainika kuwa eneo la mlipuko wa madini halipo ndani ya leseni halali, hatua za urasimishaji huchukuliwa ili kuruhusu shughuli za uchimbaji kufanyika kwa utaratibu, ikiwemo utoaji wa leseni kwa wahusika wanaokidhi vigezo. Hata hivyo, Serikali imebaini kwa masikitiko kuwepo kwa tabia inayoongezeka ya baadhi ya wachimbaji wadogo wasio waaminifu kuvamia maeneo yenye leseni halali za madini. Vitendo hivi vimesababisha migogoro, hasara kwa wawekezaji halali, pamoja na kuvuruga utaratibu wa usimamizi wa sekta ya madini. Kutokana na hali hiyo, natoa onyo kali kwa mtu yeyote au kikundi chochote kinachojihusisha na uvamizi wa maeneo yenye leseni halali kwa kigezo cha kuifanya kuwa gold rush. Tabia hiyo inakemewa vikali na kuanzia sasa ni marufuku kuvamia maeneo ya leseni za madini kwa sababu yoyote ile. Utaratibu wa utoaji wa leseni za madini upo wazi katika Sheria yetu ya Madini na Kanuni zake na ni lazima ufuatwe. Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote watakaokiuka maelekezo haya, ikiwa ni pamoja na kuwaondoa katika maeneo husika na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria. Wizara ya Madini inasisitiza kuwa maendeleo endelevu ya sekta ya madini yanategemea uzingatiaji wa sheria, nidhamu, na ushirikiano kati ya Serikali, wawekezaji, na wananchi. Hivyo, wadau wote wanahimizwa kufuata taratibu zilizowekwa na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani, afya ya jamii, na utulivu wa nchi yetu. Ndugu wanahabari, Kwa kumalizia, naomba nitoe rai kwa wawekezaji wote kwenye Sekta ya Madini kuendelea kuzingatia matakwa ya Sheria ya Madini, Sura 123. Wizara ya Madini itaendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kufanya uwekezaji wenye tija na kukuza uchumi wa Taifa letu kutokana na uvunaji wa rasilimali madini. “MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI” “ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA” 4

by: madini

Latest News
Mawaziri Afrika Wajadili Madini Mkakati

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameshiriki Mkutano wa Pili wa Mawaziri wa Madini Afrika …

by: madini on: Oct. 7, 2022, 11:20 a.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

TANZANIA TO PARTAKE FOR MAIDEN TIME IN SA’S MININ…

The Ministry of Minerals informs the public and mining sector stakeholders that Tanzania, in collab…

by: madini on: Jan. 24, 2024, 7:59 p.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals